MTANDAO wa Jinsia Tanzania (Tanzania Gender Networking Programme – TGNP) kwa kushirikiana na CARE Tanzania wametoa mafunzo ya siku tatu kwa wawezeshaji wa ngazi ya jamii katika kata ya Mtitu na Ng’uruhe, wilayani Kilolo mkoani Iringa kupitia mradi wa ‘Ustahimilivu Wake, Dunia Yetu.’
Mafunzo hayo yamewahusisha wafugaji, vinara wa masuala ya jinsia pamoja na vikundi vya wanawake kutoka vijiji vya Mtitu, Lulanzi, Luganga, Lukani na Isuka, yakilenga kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya jinsia, utunzaji wa mazingira na mbinu za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwezeshaji kutoka TGNP, Schola Makwaia, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki kupata maarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuyashirikisha katika vikundi vyao na jamii kwa ujumla, na hivyo kusaidia kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo.
Nao baadhi ya washiriki wamesema mabadiliko ya tabianchi yamekuwa yakiathiri shughuli zao za kilimo na ufugaji, ikiwemo ukame na mvua chache zinazosababisha upungufu wa malisho ya mifugo.
