Latest Posts

WAGONJWA KUBEBWA KWENYE ‘MATENGA’ TUNDURU: RAIS SAMIA ASISITIZA UWAJIBIKAJI WA VIONGOZI DHIDI YA HABARI ZA UONGO

Na Amani Hamisi Mjege.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi katika ngazi mbalimbali nchini kuhakikisha wanawajibika ipasavyo pale wanapokutana na taarifa zisizo za kweli kuhusu miradi ya serikali.

Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Tunduru, mkoani Ruvuma, Rais Samia alionesha masikitiko yake juu ya taarifa alizodai kuwa za uongo, zilizosambazwa mitandaoni hivi karibuni kuhusiana na huduma za afya katika kata ya Mchoteka, wilayani humo.

Taarifa zilizoenezwa zilidai kuwa wananchi wa Kata ya Mchoteka, Tunduru wanalazimika kusafirisha wagonjwa kwenye matenga kutokana na ukosefu wa gari la wagonjwa. Ilielezwa kuwa gari la wagonjwa lililoletwa hapo awali lilihamishwa na kupelekwa kata nyingine, huku wananchi wakitozwa gharama kubwa kwa matumizi ya gari hilo.

Kutokana na hilo, Katibu Mkuu wa chama cha ACT Wazalendo Ado Shaibu alimwomba Rais Samia kutoa mwongozo kwa halmashauri za wilaya ili kutenga fedha za kuendesha magari ya wagonjwa kwa urahisi wa wananchi.

SERIKALI YAJIBU

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alitoa majibu mbele ya Rais kuhusu suala hilo. Mchengerwa alieleza kuwa serikali, kupitia uongozi wa Rais Samia, imenunua zaidi ya magari 530 ya huduma za wagonjwa kote nchini. Aliongeza kuwa Wilaya ya Tunduru pekee ilipokea magari manne ya kuhudumia wagonjwa ambayo yamepelekwa kwenye vituo vya afya vya Nakapanya, Matemanga, Mchesi, na Nalasi.

“Mheshimiwa Rais, magari zaidi ya 300 ulinunua wewe mwenyewe na ukamkabidhi kila mbunge wa jimbo magari apeleke kwenye vituo venye changamoto katika maeneo yetu. Mheshimiwa Rais ninaomba nikutaarifu, halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ulinielekezs tulete magari manne ya kuhudumia wagonjwa kwenye sekta ya afya, magari haya yalipangwa na viongozi wa Halmashauri, yalikwenda Tunduru Kaskazini katika Kituo cha afya cha Nakapanya kilipokea gari za kuhudumia wagonjwa, kituo cha afya cha Matemanga kimepokea gari ya kuhudumia wagonjwa. Tunduru Kusini kituo cha afya cha Mchesi kimepokea gari ya kuhudumia wagonjwa, kituo cha afya cha Nalasi kimepokea magari ya kuhudumia wagonjwa”, alieleza Mchengerwa.

Waziri huyo pia alieleza kuhusu mpango wa M-Mama, ambao unalenga kusaidia usafiri wa dharura kwa wagonjwa, akisema zaidi ya shilingi bilioni 2.7 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha huduma hiyo, huku madereva wa kijamii wakipewa mikataba ya kuwahudumia wananchi katika maeneo ambayo magari ya wagonjwa hayapatikani.

RAIS SAMIA ATOA ONYO

Rais Samia alionesha kutofurahishwa na tabia ya baadhi ya viongozi kukaa kimya wakati taarifa za ‘uongo’ zinapozagaa mitandaoni, akiwataka wachukue hatua za haraka kukanusha uvumi usio na msingi.

“Suala la kuchanganya picha za kuzusha zinazorushwa katika mitandao, ndugu zangu Watanzania kama kunarushwa picha ya uongo katika mitandao, katika maeneo yetu kuna wakuu mbalimbali wapo. Lakini hakuna anayekanusha kwamba hiyo picha siyo ya leo, kwamba hiyo hospitali au hilo eneo sasa hivi liko kwenye hali hii na ikapigwa picha ikaingizwa kuondoa ule upotovu uliofanywa, sijui tunaelekea wapi? Kwamba mpaka aje Rais na mawaziri wasimame wakanushe wakati mnaozuliwa hiyo hali mpo, hii sio sawa”, alisikitishwa Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alikemea tabia ya baadhi ya watu aliowaita kuwa wenye nia ovu kutengeneza taarifa za uongo kuhusu maendeleo ya serikali, huku viongozi wakishindwa kuchukua hatua. Aliwasihi viongozi kuimarisha uwajibikaji wao na kulinda maslahi ya wananchi dhidi ya upotoshaji uliotajwa kuweza kuhatarisha imani yao kwa serikali na miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa.

Rais Samia pia alihimiza viongozi kuhakikisha huduma za afya zinaendelea kuboreshwa, akibainisha kuwa serikali itaendelea kufanya kila jitihada kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora, hasa kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!