Latest Posts

WAHARIRI WAMTAKA WAZIRI SILAA KUJITOKEZA KATIKA MATUKIO MUHIMU YA TASNIA YA HABARI

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeonesha kutoridhishwa na kitendo cha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, kushindwa kuhudhuria mikutano muhimu ya wadau wa habari.
 
Mwenyekiti wa TEF Deodatus Balile ameeleza hisia hizo Novemba 7, 2024 Jijini Dar es Salaam katika Mkutano Mkuu wa Nane wa TEF ulioanza siku hiyo, ambapo pia Waziri Silaa hakufika badala yake amemtuma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
 
“Sisi Kama Wahariri hatufurahishwi, na hatuwezi kuficha jambo hili, hatufurahishwi na Waziri wa Habari, Mawasiliano, na Teknolojia ya Habari Jerry Silaa. Alialikwa kwenye Mkutano wa PST hakwenda, alialikiwa kwenye tuzo za waandishi wa habari hakwenda, alialikwa Mbeya kwenye tukio la wadau wa habari hakwenda, na sasa Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Wahariri hajaja. Hii inaonesha kuwa Waziri hayupo tayari kushirikiana na wadau wa tasnia ya Habari” ameeleza Balile.
Balile amesema matukio mithili ya hayo ni fursa kwa wadau na Waziri kukutana na kujadili mustakabali wa tasnia ya habari, na kutokuwepo kwake ni pigo kwa ushirikiano uliotarajiwa.
 
“Kwenye matukio ya aina hii ni jukwaa sahihi kwa wadau kukutana na Waziri, na kuzungumza kwa pamoja masuala muhimu yanayohusu mustakabali wa Tasnia ya Habari, lakini tunasikitika kuwa Waziri hayupo tayari kwa ushirikiano”, ameongeza Balile.
 
Kwa upande mwingine, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nicholas Mkapa, ambaye alimwakilisha Waziri kwenye mkutano huo wa TEF, ameeleza kuwa Waziri Silaa alikuwa na majukumu mengine ya kiofisi, hivyo kumtuma kuwakilisha.
 
Balile pia alikumbusha kuwa, wakati Waziri Nape Nnauye alipokuwa Wizara ya Habari, alitoa ushirikiano wa hali ya juu kwa kuhudhuria mikutano yote muhimu ya wadau, hali iliyotajwa kuwa na tija kubwa kwa maendeleo ya tasnia.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!