Shirika la African Music/Art’s and Vocal Training Academy (AMVOTA) Kwa kushirikiana na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) wameandaa tuzo za kidini za kutambua mchango wa watu, waimbaji na viongozi wa kidini waliofanya mambo makubwa.
Akizungumzia tuzo hizo siku ya Jumatatu jijini Mwanza Mratibu wa tuzo hizo, Godbless Godfrey amesema tuzo hizo zitafanyika Juni 21, 2024 katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza zikitarajia kukusanya vijana zaidi ya 8000 huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
“Kuna watu hawajui kazi ya Fanuel Sedekia amefanyakazi kubwa ambazo zinaendelea kuishi mpaka leo nyimbo zake zinazidi kututia moyo japokuwa amesha kufa ikitokea msiba unakuta nyimbo zake zinapigwa kwahiyo tunataka tuenzi watu waliofanya makubwa kwenye injili,” amesema Godfrey
Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la AMVOTA, Profesa Paul Nyabagaka amesema tuzo hizo sio za mashindano na hazita kuwa na ubaguzi kwani zitajumuisha mathehebu mbalimbali huku wakiangalia mchango wa kila mmoja.
“Itakuwa ni historia katika jiji letu la Mwanza jambo ambalo halijawahi kutokea tangu Mwanza imekuwepo kuwakusanyisha watu katika uwanja wa Nyamagana zaidi ya vijana 8000 lakini kwa lengo kubwa kutoa tuzo kwa kutambua mchango wa watu katika huduma hii ya injili,” amesema Profesa Nyabagaka
Kwa upande wake Katibu wa Baraza la Makanisa ya Pentekoste Mkoa wa Mwanza, Dk Robert Bundara amewapongeza AMVOTA kwa kuwaleta vijana pamoja kupitia tuzo hizo na kwamba hiyo ni sehemu ya kuimarisha amani katika nchi.
“Katika uimbaji kunavipaji mbalimbali na waimbaji wengi wamekuwa wakiimba lakini hawatambuliwi uimbaji ni kazi kama kazi nyingine kwasababu wengine katika uimbaji wamefanikiwa katika kongamano hili kuwleta vijana Pamoja kuelekea kipindi hiki itakuwa ni sehemu ya kuhamasisha amani” amesema Dk Bundala