Latest Posts

WAKALA WA VIPIMO TANZANIA WAPATIWA VITENDEA KAZI VIPYA KWA UHAKIKI WA BIDHAA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa vitendea kazi vya magari kumi kwa Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) ili kuhakikisha uhakiki sahihi wa vipimo vya bidhaa viwandani kabla ya kufikishwa kwa mlaji wa mwisho nchini.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, wakati akikabidhi magari mawili kati ya magari kumi yaliyotolewa kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini, Alban Kihulla, katika kikao cha siku tatu cha watendaji wakuu na mameneja wa mikoa nchini.

Dkt. Hashil amesema kuwa wamekabidhi magari mawili, huku hatua za mwisho zikikamilishwa ili kukabidhi magari mengine nane kwa taasisi hiyo, kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi wa Wakala hao.

“Katika kikao hiki, tumepokea maagizo kutoka kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dr. Suleiman Jafo, ili tuweze kujipanga kufanya kazi kwa uadilifu na uweledi katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kila siku,” amesema.

Aidha, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Viwanda na Biashara amezindua jarida maalumu ambalo ni Mbiu ya Wakala wa Vipimo, litakalokuwa linatolewa kila baada ya miezi mitatu, kwa lengo la kuhabarisha umma kuhusu shughuli na huduma za taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo Tanzania, Alban Kihulla, amesema kuwa wamekuwa na mafunzo maalum ya kukumbushana sheria mbalimbali za vipimo. Kihulla ameongeza kuwa Wakala wa Vipimo nchini wamepokea maelekezo ya kujipanga kupitia kikao hicho ili kuongeza nguvu za ukaguzi wa bidhaa na kumlinda mlaji wa mwisho wa bidhaa zinazofungashwa nchini.

“Lengo kuu likiwa ni kukuza uchumi wa sekta mbalimbali na kusaidia wananchi wanaonunua bidhaa zinazofungashwa hapa nchini na zinazotoka nje ya nchi,” amesema Kihulla.

Wakala wa Vipimo nchini WMA wana wajibu wa kuhakiki vipimo vya bidhaa zinazofungashwa, ikiwemo urefu, uzito, na ujazo, ili kumhakikishia mlaji wa mwisho kwamba thamani ya fedha anayotoa inaendana na bidhaa anayonunua.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!