Latest Posts

WAKILI AMKINGIA KIFUA TUNDU LISSU, ‘SIONI UHAINI KWA LISSU’.

Na Josea Sinkala, Mbeya.

Wakili wa kujitegemea Ezekiel Mwampaka amesema anakubaliana na mpango wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wa kutaka kutofanyika kwa uchaguzi mkuu baadaye Oktoba 2025 kutokana na kudai kugubikwa na kasoro mbalimbali na ukosefu wa tume huru ya uchaguzi.

Wakili Mwampaka amesema hayo kwenye mahojiano yake maalumu na kituo hiki ofisini kwake jijini Mbeya akieleza pia masikitiko yake juu ya ukamatwaji wa mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Tundu Antipas Lissu unaodaiwa kutokuwa wa staha na bila kosa linaloeleweka.

Wakili huyo wa kujitegemea nchini Tanzania, amesema pamoja na kuwa hajui mbinu ambazo CHADEMA itazitumia kuzuia uchaguzi jambo ambalo ni takwa la kikatiba kwa wananchi lakini mpango huo anaona CHADEMA iko sahihi kutokana na kushamiri kwa kasoro mbalimbali kwenye chaguzi za Tanzania hususani kuminywa kwa uhuru wa vyama vya upinzani, jeshi la Polisi kuingilia masuala ya kiuchaguzi na tume ya uchaguzi kutokuwa huru kutokana na kuwa na mfumo wa chama tawala (CCM) mambo anayosema ni wazi kuwa ndiyo yamewashawishi CHADEMA kuishinikiza jamii kuungana nao kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwaka huu hadi sheria za uchaguzi zitakaporekebishwa.

Kuhusu kukamatwa kwa Lissu na tuhuma zinazomkabili wakili huyo amesema “Hapa majuzi kuna kiongozi mmoja wa CHADEMA (Tundu Lissu) amekamatwa eti kwa uhaini na makosa mengine, sasa unafikiria kwa akili ya kawaida tu Polisi kutoka Dar es Salaam hadi Mbinga mkoani Ruvuma na msafara wa magari ambao ni kodi za wananchi kulikuwa na haja gani, walishindwa nini kutafuta namba ya simu wakampigia au wakamwamwambia bwana tunakuhitaji kituo cha Polisi Dar es Salaam siku fulani tarehe fulani wanadhani Lissu angekataa hadi watumie nguvu kiasi kile?”, amehoji wakili Mwampaka na kuongeza.

“Ukiangalia ni mpango uleule kama walivyofanya kwa Mbowe (aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA Taifa) walimkamata hivi hivi na baadaye wakamuachia. Utashangaa hili suala la Lissu linapigwa kalenda mpaka uchaguzi halafu baada ya hapo mtu anaamua anajisikia kumwachia anasema muachieni, sasa muda aliopoteza utamlipa nini na haya yote ni mfumo tulio nao kikatiba. Mimi nikisoma sioni mahali kusema utawaambia watu wagomee uchaguzi au uchaguzi uzuiwe kwamba ni uhaini sijaona”, ameeleza wakili Ezekiel Mwampaka.

Pamoja na hayo ameeleza chaguzi za Tanzania kugubikwa na wizi wa kura ikiwemo maeneo ambayo kura feki na za wizi huingizwa na mara nyingine idadi ya kura kuzidi idadi ya wapiga kura jambo linalomsukuma kueleza umuhimu wa upatikanaji wa tume huru ya uchaguzi akisema tume iliyopo sasa kiongozi wake anayeteua viongozi wa tume ni mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!