Wakili Paul Kisabo amemuandikia barua Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) wa Tanzania akitaka majibu juu ya upelelezi wa kupatikana kwa Deusdedith Soka, Jacob Mlay na Frank Mbise, waliotekwa.
Kisabo amesema kuwa barua hiyo, aliyoiwasilisha Februari 7, 2025, ilipokelewa rasmi na ofisi ya IGP Februari 10, 2025. Wakili huyo anataka ufafanuzi wa utekelezaji wa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, ambayo ililitaka Jeshi la Polisi kufanya upelelezi wa kuwatafuta watu hao.
“Ikumbukwe kwamba Agosti 22, 2024, nikiwa wakili wa Deusdedith Soka, nilifungua shauri la jinai namba 23998 kudai kuwa Soka, Jacob Mlay na Frank Mbise waachiliwe huru baada ya kutekwa,” amesema Kisabo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, Agosti 28, 2024, Mahakama Kuu ya Tanzania, Masijala ya Dar es Salaam, iliwaagiza polisi kufanya upelelezi wa kuwatafuta watu hao, lakini hadi sasa hakuna taarifa rasmi kuhusu utekelezaji wa uamuzi huo.
“Sasa ni zaidi ya miezi mitano bila taarifa yoyote rasmi kuhusu utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu. Maamuzi ya Mahakama Kuu ni lazima yatekelezwe kikamilifu, na kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ni kosa kutokutekeleza maamuzi ya mahakama,” amesema Kisabo.
Hadi sasa Jeshi la Polisi halijatoa tamko rasmi kuhusu hatua iliyofikiwa katika upelelezi wa sakata hilo.