Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) Wakili Onesmo Olengurumwa, amesema kwamba watetezi wa haki za watoto wana jukumu kubwa la kusaidia katika jitihada za kukabiliana na matukio ya ukatili kwa watoto, hasa kipindi hiki ambacho kumekuwepo na taarifa za matukio mengi ya utekaji na vitendo vya ulawiti na ubakaji kwa watoto.
Wakili Olengurumwa ameeleza hayo Julai 31, 2024 katika semina ya siku mbili inayolenga kuwajengea uwezo watetezi hao kwenye masuala mbalimbali ikiwamo ya kisera na kisheria.
“Tunafahamu hali ya ulinzi wa mtoto nchi hii imekuwa na changamoto nyingi sana, Ripoti ya Jeshi la Polisi juzi ilionesha utekaji umekuwa mkubwa, kwa mfano mwaka jana tu watoto zaidi ya 73 kwa mujibu wa ripoti hiyo, tumeona masuala ya ulawiti na ubakaji yote yamekuwa matatizo makubwa ambayo hawa Watetezi wa Haki za Binadamu wanapaswa kukemea, kufuatilia na hata kuwajibisha zile taasisi ambazo zinahusika na ulinzi wa haki za Kiraia” Ameeleza Wakili Olengurumwa.
Aidha Mratibu wa Kitaifa wa Tanzania Children Rights Forum, Ombeni Kimaro, amesema kuwa uelewa mdogo uliopo katika jamii juu ya masuala yanayohusu haki za watoto ni sababu inayosababisha vikwazo katika ulinzi wa haki za watoto.
Pia amewaasa wazazi, walezi na jamii kwa pamoja kuwa mfano bora katika kuhakikisha wanasimamia na kulinda haki za watoto, ambapo amesema kwa upande wao wamekuwa wakichukua hatua mbalimbali kuhakikisha haki za mtoto zinalindwa ikiwamo kushirikiana na serikali.
Washiriki wa semina hiyo wametokea mikoa nane ikiwamo mkoa wa Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Singida, ambapo yatahitimishwa tarehe 1 Agasti 2024.