Wakulima wa zao la mbaazi katika mkoa wa Mtwara wameiomba Chama Kikuu cha Ushirika kinachohudumia wilaya za Mtwara, Masasi, na Nanyumbu (MAMCU) kuendelea na mnada wa mbaazi kwa sababu bado sehemu kubwa ya mbaazi hizo zipo mashambani.
Wakulima hao wamewasilisha ombi lao katika mnada wa saba wa mbaazi uliofanyika Septemba 6, 2024, katika Tarafa ya Mikindani.
Walisema kuwa mavuno ya mbaazi bado yanaendelea mashambani na hawajamaliza kuvuna, hivyo ni muhimu mnada huo uendelee ili wasikose fursa ya kuuza mazao yao.

Katika mnada huo, tani 1,338 za mbaazi ziliuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 1,760 na bei ya chini ya shilingi 1,693. Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Prince Mng’ong’o, amewashauri wakulima kuzingatia ubora wa mazao yao wanapoendelea kukusanya mbaazi, akisisitiza kuwa mnada bado unaendelea.
Afisa Masoko wa MAMCU, Neema Mavele, alieleza kuwa hadi sasa wakulima wamepokea malipo ya shilingi bilioni 36 kwa mbaazi zilizouzwa kupitia mnada huo. Pia aliwasihi wakulima kuendelea kuzingatia ubora wa mbaazi ili kufaidika zaidi na soko hilo.
Mnada huo unaendelea kuwa muhimu kwa wakulima wa Mtwara, wakitegemea kuuza mbaazi zao kwa bei nzuri ili kupata manufaa ya moja kwa moja kutokana na juhudi zao za kilimo.