Mrajisi na Mtendaji Mkuu kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) Dkt. Benson Ndiege amewataka wakulima kuhakikisha wanapopeleka mizigo yao kwa ajili ya kupima wahakikishe wanapima kupitia mizani ya kidijitali ili kuepuka kupunjwa mazao yao.
Hayo ameyazungumza Septemba 29, 2024 alipozungumza na waandishi wa habari kuelekea kwenye ufunguzi wa kiwanda cha Kubangulia korosho kinacho simamiwa na Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (TANECU) kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Newala kijiji cha Mnovo Mkoani Mtwara.
Amesema baadhi ya vyama vya ushirika (AMCOS) na watendaji wa vyama hivyo hawataki kutumia mizani hizo na wanaziharibu ili zisifanye kazi kama inavyotakiwa ili kuendelea kumpunja mkulima.
Aidha amewataka viongozi wa Amcos na vyama vikuu vya ushirika wahakikishe kuwa mizani hizo zinatumika kwani zimekuja kwa ajili ya kumlinda mkulima.
Amesmea utumiaji wa mizani hizo unalengo la kuongeza uwazi na kumlinda mkulima ili aweze kupata fedha kulingana na kazi aliyoifanya hivyo mkulima anapokwenda kupima taarifa za mzigo wake zinawafikia wahusika ikiwemo mkulima mwenyewe.
Sambamba na hilo kuelekea kwenye msimu wa korosho ambao minada inakwenda kuanza rasmi Oktoba 11,2024, Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Francis Alfred amewaomba wanunuzi kutoa bei nzuri itayokuwa na manufaa makubwa kwa wakulima na waweze kuwa na ustawi wa kuhudumia zao hilo la korosho.
“Tutasimamia zaidi kwenye upande wa waendesha ghala kuhakikisha kwamba wanazingatia maelekezo, mwendesha ghala ambae ataenda kinyume cha utaratibu kutozingatia taratibu za zao,kuhakikisha zao tunalolipata linalokuwa zuri”Amesema Francis
Amewaomba wanunuzi wa zao hilo wahakikishe kabla ya minada kuanza wawe wamekamilisha usajili ili waweze kushiriki kwenye minada kwani hakutakuwa na mnunuzi yoyote ambaye hajakamilisha taratibu za usajili kushiriki kwenye minada.
Akijibu swali kuhusu soko la awali, Mkurugenzi huyo wa Cbt amesema kwa sasa wameboresha zaidi na msimu huu korosho zote zinazonunuliwa kupitia soko la awali italosimamiwa chini ya vyama vikuu hivyo na malipo yote kwenda kwa wakulima yatasimamiwa na vyama vikuu.
Chama Kikuu Cha Ushirika kinachohudumia Wilaya za Newala na Tandahimba (TANECU) imefanikiwa kujenga kiwanda cha kubangulia korosho chenye uwezo wa kubangua tani 3,500 kwa mwaka chenye thamani ya Sh bilioni 3.4 kinachotarajiwa kuzinduliwa Oktoba 1,2024 na Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
Ujenzi wa kiwanda hicho ni katika kuendeleza juhudi za serikali ifikapo 2030 korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa hapa nchini na kuongezewa thamani.