Halmashauri zote tisa mkoani Mtwara zimetakiwa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kutekeleza programu jumuishi ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa ngazi zote.
Hayo yamezungumzwa na Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara Bahati Geuzye kwenye kikao cha tathimini ya utekelezaji shughuli za programu jumuishi ya taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto (PJT-MMMAM).
Aidha, amewataka kuweka mazingira wezeshi kwenye maeneo yao ya kazi ili kuwawezesha wananchi wanaohudumiwa kwenye ofisi zao waweze kupata elimu hiyo ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuwapa vipeperushi na kutumia mikutano mbalimbali.
Hata hivyo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kupitia maafisa maendeleo kuhakikisha wanafanya ukaguzi kwenye vituo vyote vya kulelea watoto wadogo mchana ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa watoto zinazingatia miongozi ya malezi ya mtoto.
Lazaro Ernest Meneja Mradi wa Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) amesema ni muhimu kuwekeza kwa mtoto mdogo kuanzia umri wa mwaka 0 hadi 8 ili kupata matokeo chanya kwa jamii na taifa
“Umri huo ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto kwa kuwa huenda kwa haraka zaidi pia watoto hujifunza kwa haraka zaidi, na kwa kipindi cha miaka 6 ya mwanzo ubongo ufikia 90% ya ukuaji wake”, amesema Ernest.
Amesema Tanzania ina takribani 27% ya watoto chini ya umri wa miaka 8 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, pia 53% wapo kwenye hatari ya kutofikia ukuaji timilifu katika eneo la afya, ujifunzaji wa awali na ustawi wa kijamii.
Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Jalmadini Salim amesema Mwenyezimungu ametoa maelekezo kutoka kwenye kitabu tukufu Qur’an yanayohusu masilahi na uangalizi wa mtoto ambao ndio tegemeo na heshima ya taifa na kila nchi, huku akiwataka kutilia mkazo ili kupata watoto wanaohitajika.
Kikao hicho cha tathimini kimefanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani humo na kushirikisha viongozi mbalimbali kutoka kwenye Halmashauri hizo zote ndani ya mkoa huo wakiwemo maafisa ustawi wa jamii, maafisa maendeleo, waganga wakuu, maafisa lishe na wengine.