Latest Posts

WAKUU WA VYOMBO VYA HABARI, WAHARIRI WAANDAMIZI WAHIMIZA AMANI KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

Wakuu wa vyombo vya habari na wahariri waandamizi nchini wamewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kuepuka kauli au matendo yenye mwelekeo wa uchochezi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Wametoa rai hiyo Kupitia azimio lao la pamoja ambalo limesomwa leo jijini Dar es Salaam leo Jumamosi Oktoba 25, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa ITV/Radio One, Joyce Mhavile, katika mkutano uliowakutanisha wakuu wa vyombo vya habari, wahariri waandamizi na waandishi kutoka taasisi mbalimbali za habari nchini.

Akisoma azimio hilo kwa niaba ya wakuu wa vyombo vya habari nchini na Wahariri Waandamizi, Mhavile amesema Tanzania imepata heshima kubwa ya kuwa kisiwa cha amani barani Afrika, kutokana na misingi imara iliyowekwa na waasisi wa taifa, ikiwemo utamaduni wa kutatua tofauti kwa njia ya majadiliano na siasa za hoja badala ya vurugu.

“Watanzania tuna wajibu wa kuendelea kujenga demokrasia yetu kwa majadiliano na hoja, tukipingana bila kupanga kupigana.” alisema Mhavile 

Akizungumza baada ya tamko hilo kusomwa, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema wakuu wote wa vyombo vya habari nchini wamesaini azimio hilo, ambalo linapaswa kuwa rejea muhimu kwa vyombo vya habari katika kipindi chote cha kuelekea uchaguzi.

“Wakuu wote tumesaini azimio hili, na tunaviasa vyombo vya habari vilitumie mara kwa mara kwa kadri inavyowezekana kuelekea uchaguzi mkuu.” alisema Balile 

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dkt. Ayub Rioba Chacha, amewahimiza waandishi wa habari na taasisi za habari kuhakikisha azimio hilo linasambazwa kwa wananchi, ili kuimarisha umoja na kwa kuwa ni suala ambalo lina maslahi ya Taifa.

“Naamini waandishi wa habari mtaendelea kusambaza azimio hili kwa Watanzania, kwa kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuhakikisha vinawasilisha kwa wananchi kile kinachokuwa na maslahi kwa taifa.”

Wakuu hao wa vyombo vya habari na Wahariri Waandamizi wamesema, vyombo vya habari vina wajibu wa kulinda amani na umoja wa taifa, kwa kuripoti kwa uadilifu na kuepuka lugha za chuki, ambazo zinaweza kuchochea migawanyiko ya kijamii au kisiasa.

Tamko hilo limeonya juu ya ongezeko la kauli za uchochezi katika majukwaa ya kisiasa na mitandao ya kijamii, likibainisha kuwa ni hatari kwa umoja wa kitaifa na linaweza kuathiri amani ya nchi kama ilivyotokea katika mataifa mengine ya Afrika.

Sehemu ya tamko hilo imesema: “Kauli zinazohamasisha vurugu, kuchoma vituo vya mafuta au kushambulia taasisi za umma ni makosa kisheria na kinyume na utu wa Mtanzania.”

Katika hatua nyingine, wamekumbusha historia ya mataifa yaliyotumbukia katika machafuko kama Rwanda, Kongo, Somalia, Liberia na Sudan, wakibainisha kuwa machafuko hayo yalianza kwa kauli za uchochezi zilizopandikizwa kupitia vyombo vya habari na propaganda za kisiasa.

Aidha, wameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kimbilio la wakimbizi kutoka mataifa yenye migogoro kutokana na misingi ya amani na maelewano, na hivyo Watanzania wanapaswa kulinda urithi huo kwa gharama yoyote.

“Tukatae kuhudhuria karamu ya uchochezi wenye lengo la kutushawishi kulewa uwendawazimu wa kihalaiki ambao unaweza kulisambaratisha taifa letu.” imesema sehemu ya tamko hilo 

Azimio hilo limehitimishwa kwa wito wa pamoja kutoka kwa Wakuu wa Vyombo vya Habari nchini na wahariri wote, wakisisitiza umuhimu wa kuendeleza mijadala yenye kujenga taifa, na likafungwa kwa maneno: “Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Afrika.”

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!