Latest Posts

WALIMU WA HALMASHAURI YA WILAYA YA GEITA WATAKIWA KUONGEZA UFAULU WA WANAFUNZI

Walimu wa Halmashauri ya wilaya ya Geita wametakiwa kuongeza juhudi katika kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi ili kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne ambalo limekuwa kikwazo kwao kuendelea na masomo katika vyuo vya kati

Katibu Tawala wa mkoa wa Geita Mohammed Gombati ametoa wito huo wakati wa hafla fupi ya kuwapongeza walimu wa shule za sekondari zilizofanya vizuri mwaka 2023, ambapo amewataka walimu kuhakikisha wanafunzi wanaofaulu kwa kupata madaraja ya chini kama vile daraja la nne wanapungua ili kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na vyuo vya kati

“Ni jukumu letu kama walimu kuhakikisha ufaulu wa wanafunzi unakuwa bora zaidi, na kupunguza idadi ya wale wanaopata madaraja ya chini, hii itasaidia kuwa na wanafunzi wengi zaidi wanaoweza kuendelea na masomo ya juu katika vyuo vya kati” -Gombati

Katika kipindi cha mwaka 2022/23 jumla ya shule za sekondari 29 zimeanzishwa katika wilaya ya Geita hatua iliyochangia kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi

Afisa elimu sekondari wa wilaya ya Geita Hossana Nshulo ameeleza kuwa ufaulu wa wanafunzi umeongezeka kutoka asilimia 82 mwaka jana (2023) hadi asilimia 87 mwaka huu (2024) akionyesha kuwa kuna maendeleo makubwa yaliyopatikana

“Kuanzishwa kwa shule hizi mpya kumekuwa na athari kubwa chanya katika ufaulu wa wanafunzi wetu, tunajivunia kuona ufaulu ukiongezeka mwaka hadi mwaka” -Nshulo

Walimu walioshiriki kwenye hafla hiyo pia wametoa maoni yao, wakiiomba serikali kuendelea kuwapa motisha ili kuimarisha ari yao ya kufundisha, walimu hao wamesema kuwa motisha ni muhimu kwao kwani inawapa nguvu ya kuendelea kufundisha kwa bidii jambo linaloleta matokeo bora kwa wanafunzi

Angel Mfugale ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Magenge amesisitiza umuhimu wa walimu kupewa motisha zaidi ili kusaidia wanafunzi kufikia malengo yao ya kielimu, wakati huohuo Patrick Ntayembala ambaye ni mwalimu wa shule ya sekondari Bugarama ameongeza kuwa walimu wanapaswa kutumia mbinu bora za ufundishaji huku wakipata msaada wa serikali kwa vifaa na motisha muhimu

Wito huo unalenga kuboresha elimu katika wilaya ya Geita na kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata nafasi zaidi za kujiendeleza kielimu na kitaaluma

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!