Wanachama 45 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Lindi na viongozi wao wamejiunga na chama cha ACT Wazalendo, na kupokelewa Julai 11, 2024 na Makamu Mwenyekiti wa ACT Bara Isihaka Mchinjita ambaye amewapongeza na kuwaambia kuwa wamechagua jukwaa sahihi lenye majawabu ya matatizo na changamoto zinazowakabili watu wa Lindi.
Viongozi waliojiunga ACT ni pamoja na Mwenyekiti CHADEMA mkoa wa Lindi Zainab Lipalapi, Mwenyekiti Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) mkoa wa Lindi Said Mzee, Katibu wa Jimbo Musa Rwegoshora, Mwenyekiti wa Wazee Jimbo Bakari Likaku, Mweka Hazina wa Jimbo Mohamed Mandoyo, na Mwenyekiti BAVICHA Jimbo Doa Omari.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake Rwegoshora amesema mkoa wa Lindi lazima utoke mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ili itoke ni wajibu kwa Wanalindi kuwa na jukwaa moja la upinzani ambalo amelitaja kuwa la ACT-Wazalendo.
Katika hatua nyingine Makamu Mwenyekiti ACT bara Isihaka Mchinjita amezungumzia uduni wa huduma mbalimbali za kijamii nchini ikiwamo ile ya afya akiitaja kuwa yenye gharama kubwa ukilinganisha na maisha ya Watanzania wengi.
“katika nchi hii mtu hutibiwi bila ya malipo. Watanzania wanakufa kwa kushindwa kumudu gharama za afya. Sera ya CCM, afya ni kwa malipo. Kwa hivyo tunawajibu sisi sote kuindosha CCM madarakani” Ameeleza Mchinjita.