Mkuu wa Wilaya ya Songwe Mhe. Solomon Itunda, amewaagiza watendaji wa vijiji, kata na waratibu elimu kata kuhakikisha wanafunzi wote ambao bado hawajaripoti shuleni wanaripoti kabla ya Februari 10, 2025.
Mhe. Itunda ametoa maagizo hayo wakati wa kikao maalumu cha tathmini ya hali ya uripoti wa wanafunzi katika mwaka wa masomo 2025 kilichofanyika wilayani Songwe.
Katika kikao hicho ambacho kimewahusisha kamati ya usalama wilaya, Ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri, wakuu wa Divisheni na vitengo wa Halmashauri ya wilaya ya Songwe, watendaji kata, maafisa elimu kata na watendaji wa vijiji, kimefanya tathmini ya hali ya uripoti wa wanafunzi wa elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza katika kata zote 18 za Wilaya ya Songwe.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Itunda amesema mpaka sasa wanafunzi wa kidato cha kwanza wameripoti asilimia 78 asilimia 22 wakiwa bado hawajaripoti, darasa la kwanza asilimia 87 walioripoti ikiwa bado asilimia 13 huku wanafunzi wa awali wakiripoti asilimia 77 na asilimia 23 wakiwa bado.
Amewataka watendaji hao kufanya operesheni za kuwatafuta wanafunzi ambao hawajaripoti katika kata zao kuhakikisha wanakwenda kuanza masomo wanayostahili.
Pamoja na hayo, pia DC Itunda amewaagiza watendaji hao kuhakikisha shule zote zinaendelea kutoa chakula kwa wanafunzi shuleni.
Amesema njema ni kwamba mpaka sasa shule zote za Wilaya yake zinatoa chakula kwa watoto kwa asilimia 100 kwa wanafunzi hivyo kuweka mikakati endelevu itakayosaidia utoaji wa chakula ikiwa ni njia mojawapo ya kuinua taaluma wilayani Songwe.