Masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) yameendelea kuonesha umuhimu wake katika kuwaandaa wanafunzi kujitegemea na kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku. Hayo yamebainika wakati wa mahafali ya nne ya kidato cha sita katika shule ya sekondari ya Tumaini Senior, ambapo wanafunzi 56 walihitimu masomo yao.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Naini Koimereck alieleza kuwa kupitia masomo ya STEM, wanafunzi wamepata maarifa na ujuzi utakaowasaidia si tu katika maisha ya chuo, bali pia katika kuchangia maendeleo ya jamii zao. Alisema kuwa masomo ya STEM yametuwezesha kuwa wabunifu na kutambua changamoto za kijamii kisha kuzipatia suluhisho kwa njia za kitaalamu.
Wahitimu hao 56 walikuwa wakisomea michepuo mbalimbali ya sayansi na sayansi jamii, ambapo wavulana walikuwa 25 na wasichana 31.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hiyo, Modest Bayo, alieleza kuwa shule imejikita katika kutoa elimu bora kwa lengo la kuwaandaa vijana kukabiliana na ushindani wa kitaifa na kimataifa. Alisema kuwa kupitia uwekezaji kwenye miundombinu ya kisasa na walimu wenye uwezo, shule imefanikiwa kuwajenga wanafunzi kielimu na kimaadili. Aliongeza kuwa wanatambua dunia ya leo inahitaji watu waliobobea katika masuala ya sayansi na teknolojia, ndiyo maana shule yao imeweka mkazo katika kutoa maarifa ya kisasa kwa wanafunzi.
Wahitimu kadhaa walieleza matumaini yao makubwa ya kuendelea na masomo ya juu na kutimiza ndoto zao. Mmoja wa wahitimu alisema kuwa anapenda masomo ya sayansi na anatumaini atafaulu vizuri ili aweze kujiunga na chuo kikuu na kutimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walimu, na wageni mbalimbali waalikwa, ambapo kulikuwa na burudani, hotuba, na utoaji wa vyeti kwa wahitimu waliofanya vizuri zaidi katika masomo yao.