Latest Posts

WANAHABARI WAASWA KWENDA SAMBAMBA NA KASI YA TEKNOLOJIA KWA UMAKINI

Waandishi wa habari mkoani Mtwara wameaswa kuweka kipaumbele cha juu katika uthibitishaji wa taarifa wanazozikusanya na kuzisambaza, wakitakiwa kuona hatua hiyo kama msingi mkuu wa kulinda uaminifu wa kazi zao pamoja na ustawi wa jamii.

Hayo yamejiri katika warsha ya siku moja iliyoandaliwa na Taasisi ya Jamii Africa, iliyowakutanisha wanahabari wapatao 25 kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wao katika mbinu za kisasa za kuhakiki taarifa.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Afisa Programu wa taasisi hiyo, Edwin Chaina, alisisitiza kuwa katika zama hizi za kasi ya teknolojia, upatikanaji wa taarifa ni rahisi lakini changamoto kubwa imebaki kwenye kuzithibitisha kabla ya kuzifikisha kwa umma. Alieleza kuwa uandishi wa habari unaowajibika lazima ujikite katika ukweli uliothibitishwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kwa jamii.

Aliongeza kuwa taarifa zisizohakikiwa zinaweza kupotosha umma na kusababisha maamuzi yasiyo sahihi, hali inayoweza kudhoofisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Hivyo, aliwataka waandishi wa habari kutumia mbinu sahihi na vyanzo vya kuaminika katika kila hatua ya ukusanyaji na uchakataji wa taarifa.

Kwa upande wao, washiriki wa warsha hiyo walieleza kuwa mafunzo hayo yamewapa mwanga mpya kuhusu umuhimu wa kufuatilia kwa kina kila taarifa wanayoipata, pamoja na kuthibitisha ukweli wake kabla ya kuichapisha au kuisambaza.

Walisisitiza kuwa kuzingatia maadili hayo kutasaidia kupunguza upotoshaji wa taarifa na kuimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya habari, ambavyo vina jukumu la kutoa taarifa sahihi, zilizothibitishwa na zenye kuaminika wakati wote.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!