Latest Posts

WANAHABARI WATAJWA NGUZO KUU KATIKA UHAMASISHAJI WA MABADILIKO YA TABIANCHI

Wanahabari nchini Tanzania wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuuhabarisha umma kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi na namna yanavyoweza kuwaathiri wananchi, sambamba na kuonyesha fursa zilizomo katika kukabiliana na changamoto hizo.

Wito huo umetolewa hivi karibuni wakati wa mafunzo maalum ya siku tatu (Oktoba 22–24, 2025) kwa waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya redio, magazeti na mitandao ya kijamii, yaliyofanyika mkoani Morogoro kuelekea mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi (COP30) utakaofanyika Novemba 10–21, 2025, mjini Belem, Brazil.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Media Foundation (TMF), Danstan Kamanzi, amesema mpango huo wa mafunzo unalenga kuongeza ubora wa uandishi wa habari za tabianchi na kuhakikisha taarifa zinazoandikwa zinaibua mijadala ya kisera na uwajibikaji katika utekelezaji wa mikakati ya kitaifa.

“Tunataka kuona waandishi wanakuwa na uelewa wa kina kuhusu ajenda za COP30, ili waandike habari zenye ushawishi, zinazoelimisha na kuhamasisha hatua kwa jamii. Hii ni nafasi ya kuonyesha uwezo wa vyombo vya habari katika kuibua mijadala yenye manufaa kwa taifa, alisema Kamanzi.

Kwa upande wake, Meneja Uendeshaji kutoka Climate Action Network Tanzania (CAN), Bonaventure Mchomvu, amesema mafunzo hayo ni hatua muhimu ya kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye tafsiri ya kitaifa kuhusu maamuzi yatakayofikiwa katika mkutano wa COP30.

Ameeleza kuwa Tanzania inakwenda kwenye mkutano huo ikiwa na maazimio zaidi ya 12 yanayohusiana na juhudi zake katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuimarisha ustahimilivu wa jamii, na kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Mabadiliko ya tabianchi hayana mipaka ya kisiasa. Tanzania, kama nchi inayoendelea, imeweka nguvu kubwa katika ustahimilivu wa jamii na kupunguza uchafuzi wa anga. Sera, kanuni na mikakati iliyopo inaonyesha dhamira ya kweli ya taifa letu katika kukabiliana na changamoto hizi,”, alisema Mchomvu.

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wameishukuru TMF kwa kuwajengea uwezo wa kuripoti kwa weledi juu ya masuala ya tabianchi.

Khadija Omary Mazezele, mwanahabari kutoka Tabora, alisema mafunzo hayo yamemsaidia kujifunza mbinu bora za kusaidia jamii kuelewa maana na manufaa ya mkutano wa COP30.

“Nitawaelimisha wananchi juu ya namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri kilimo na mikakati ya wakulima kukabiliana nayo. Nimepata maarifa yatakayowezesha kuripoti kwa ufanisi zaidi,” alisema.

Naye Jimmy Kiango, mwanahabari wa mazingira kutoka Dar es Salaam, alisema mafunzo hayo yamemwezesha kuelewa kwa undani umuhimu wa mikutano ya COP na jinsi ya kuwajengea Watanzania uelewa kuhusu nafasi ya nchi yao katika maamuzi ya kimataifa.

“Ninaamini nitakuwa daraja kati ya wananchi na maamuzi ya COP. Kupitia habari nitakazoandika, Watanzania wataweza kufahamu namna maamuzi haya yanavyotugusa na jinsi tunavyoweza kuchukua hatua,” alisema Kiango.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!