Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo Wella, amewahimiza waandishi wa habari mkoani Tabora kuongeza maarifa na ujuzi wao katika tasnia ya habari ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia, ikiwemo matumizi ya akili Unde (AI), kwa lengo la kuboresha ubora wa taarifa wanazozitoa kwa umma.
Bi. Wella ametoa wito huo wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo wanahabari yaliyoandaliwa na Mtandao wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Tabora (TMN). Amesema kuwa maendeleo ya teknolojia yameleta mabadiliko makubwa katika ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa habari, hivyo ni muhimu kwa wanahabari kuendelea kujifunza ili kubaki kuwa na ushindani na kuaminika.

Aidha, amewataka wanahabari kufanya uchunguzi wa kina kabla ya kuchapisha au kurusha taarifa, ili kuhakikisha wanatoa habari sahihi, zilizothibitishwa na zenye kukidhi vigezo vya taaluma ya uandishi wa habari. Amesisitiza kuwa uchunguzi wa kutosha utasaidia kuepusha upotoshaji na kuongeza imani ya jamii kwa vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Katibu wa Mtandao wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Tabora, Bi. Stephanie Laisson, amesema mafunzo hayo ambayo hufanyika kila mwaka yanalenga kuwajengea uwezo wanahabari kwa vitendo, sambamba na kuwapa fursa ya kubadilishana uzoefu kuhusu changamoto na mbinu bora katika kazi zao za kila siku.
Baadhi ya wanahabari waliohudhiria mafunzo hayo wamesema mafunzo waliyoyapata yana umuhimu mkubwa katika kutekelezaji wa majukumu yao ,wakiomba yawe endelevu kwa mustakali wa maendeleo katika tasnia ya habari kwa ujumla.
Akifunga mafunzo hayo, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Tabora, Bw. Gulamu Dewji, amewataka wanahabari kuyatumia kwa vitendo mafunzo waliyopata ili kuboresha utendaji wao na kuendelea kutoa mchango chanya katika maendeleo ya jamii.