Wakazi wa Mtaa wa Kiyangu   ‘A’ na ‘B’ Kata ya Shangani Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wameiomba serikali kutengeneza miundombinu rafiki itakayosaidia maji yasituame sehemu moja na kusababisha athari mbalimbali kwa wananchi.
Wakizungumza na Jambo TV kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema changamoto kubwa inayosababisha kutokea mafuriko kila mwaka katika mitaa hiyo ni kukosekana kwa mifereji ambayo ingesaidia kuelekeza maji baharini na kuwaepusha na changamoto hiyo.
Cosmas Agroni, mkazi wa mtaa huo, amesema kutokana na athari zilizojitokeza ameendelea kuiomba serikali kutengeneza barabara za mitaa ambazo zitakuwa na mitaro itayosaidia kuwaepusha wananchi hao athari zitokanazo na kujaa kwa maji kwenye makazi yao.
Mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Mtwara, Naftal Agawa amewasihi wanafunzi wenzake kutafuta maeneo rafiki ya kupanga ili kuepukana na majanga wanayoyapata ambayo yatasababisha kufeli mitihani ikizingatiwa maafa yametokea na mitihani inaendelea.
“Kwa wanafunzi ambao wanaishi nje ya chuo, huu ndiyo wakati sahihi wa kuchagua sehemu za kuishi ambazo ni salama kwasababu siyo kila sehemu unaweza kuishi, kama hapa tushapoteza muda mwingi kwa ajili ya hili janga na kwa baadhi ya wanafunzi mitihani inaendelea”, amesema Agawa
Naibu Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Sixmund Lungu amesema kuwa Manispaa itashirikiana na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini Wilaya ya Mtwara (TARURA) katika kuweka mikakati ya kuimarisha miundombinu ya barabara na mifereji ili kupunguza athari zitokanazo na mvua.