Wakazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani mkoani Mtwara wametakiwa kuwa na bima ya afya ili kuepukana na gharama za matibabu na waweze kuwa na uhakika wa matibabu.
Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Jimbo CCM Mtwara Mjini 2020-2025 unaohusu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, mbunge wa jimbo hilo Hassan Mtenga amesema wananchi wengi hawana bima hali inayopelekea familia nyingi kuchangishana pesa kwa ajili ya matibabu pale inapotokea mwanafamilia kuumwa.
Pia wajiwekee utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara ili kujua hali za afya na badala yake waache kutumia dawa bila kufanya vipimo.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mtwara mjini, Salum Naida amewataka viongozi wa vyama pinzani kuondokana na siasa za kufarakanisha wananchi na badala yake kufanya siasa ambazo wananchi wanahitaji kuona matokeo bora.
“Wanamtwara wanahitaji viongozi wa vyama wanao tetea na kusimamia maendeleo ya wananchi, tuondokane na siasa uchwara ili wananchi wawapende ” Amesema Naida.
Hata hivyo amewataka viongozi wazingatie ajenda ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2024, na kuachana na ajenda nyingine ambazo wakati wake haujafika.
“Ajenda iliyoko mbele yetu ni uchaguzi wa serikali za mitaa, sitopenda kwa niaba ya kamati ya siasa kusikia huko kwenye kata zenu mmeacha ajenda ya uchaguzi wa serikali za mitaa mnabeba ajenda ya udiwani, ubunge hivi vitu bado mpaka leo bado hata wenyeviti wa serikali za mitaa tunawatambua walioko madarakani.”Amesema Naida.