Katika kuadhimisha Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkoa wa Tabora umefanya shughuli kubwa ya usafi wa mazingira na upandaji wa miti zaidi ya 24,000 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, huku wakazi wakihimizwa kuzingatia usafi kama sehemu ya juhudi za kupambana na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu na Malaria.
Akizungumza baada ya zoezi hilo lililofanyika katika Soko la National lililopo Kata ya Kitete, Manispaa ya Tabora, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alisema kuwa usafi wa mazingira ni jukumu la kila mmoja na linapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila siku.
“Tunapoadhimisha miaka 61 ya Muungano, tunatambua kuwa mazingira safi ni sehemu ya maendeleo endelevu na ustawi wa jamii yetu. Tuendelee kushirikiana kuimarisha afya zetu na mustakabali wa vizazi vijavyo,” amesisitiza Dkt. Mboya.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Tabora, Bw. Emmanuel Stanley, ameeleza kuwa Manispaa ya Tabora inalenga kupanda zaidi ya Miti milioni moja katika mwaka wa fedha 2024/2025. Hadi sasa, zaidi ya Miti laki tisa tayari imeshapandwa, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha mazingira ya Mkoa wa Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Bw. Mohamed Mtulyakwaku, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, aliwataka wananchi wote kuwa na desturi ya kufanya usafi wa mazingira kila mwisho wa wiki. Amesema kuwa: “Watakao kaidi agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria ili kuhakikisha Tabora inakuwa safi na salama kwa wote.”
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanyika rasmi Aprili 26, 1964, ni tukio muhimu ambalo liliunganisha nchi mbili huru; Tanganyika na Zanzibar, na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sherehe za mwaka huu zinaendelea kuenzi misingi ya Muungano kwa kuchochea mshikamano, maendeleo na ustawi wa taifa.