Na Helena Magabe
Tangu mchakato wa uchukuaji fomu za kuwania ubunge ulivyoanza Juni 28,2025, wananchi katika Jimbo la Tarime Vijijini walikuwa wakisubiria kwa shauku kubwa kuona endapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Eliakimu Chacha Maswi atachukua fomu kuwania ubunge katika jimbo hilo, kulikuwa na sintofahamu miongoni mwa wananchi baada ya kila siku kumalizika bila kupata taarifa yoyote juu ya kiongozi huyo kuchukua fomu,huku jina lake pamoja na baadhi ya majina ya watiania yakizua mjadala mpana jimboni humo na hasa kwenye mitandaoni ya kijami
Awali tafiti zilionesha kuwa matarajio ya baadhi ya wananchi wengi yalikuwa kwa Kiongozi huyo ambaye alikuwa akipewa nafasi ya juu na kubwa toka kwa Wananchi wa maeneo mbalimbali jimboni humo, wakitarajia atachukua fomu na jina lake litarudi kisha atagombea na pengine kushinda kinyang’anyiro hicho cha ubunge.
Hii ni kutokana na umaarufu wake na mchango aliokuwa nao katika kufanya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo kusaidia upatikanaji wa umeme katika maeneo kadhaa ya vijijini.
Hata hivyo, tofauti na matarajio ya wengi, Mzee Maswi hadi Julai 2, 2025 zoezi linafungwa hakujitokeza kuchukua fomu ingawa kiongozi huyo mkubwa katika wizara nyeti hakuwahi kutamka popote kuwa anawania nafasi hiyo isipokuwa taarifa za chini kwa chini toka kwa watu wake wa karibu zilienea jimboni kwake na kwenye mitandai ya kijamii na Wananchi kuonyesha shauku kubwa kwake akifatiwa na Nyambari Nyangwine ambaye alionekana kumkaribia.
Baada ya Maswi kutoshiriki zoezi la uchukuaji fomu imezuka minong’ono na manungu’uniko huku wengine wakimlilia kuwa ndiye alikuwa chaguo lao na kwa sasa wamebaki njia panda wasijue waelekee wapi kwani waliyemtarajia amewaacha njia panda pamoja na maswali mengi vichwani mwao.
“Tulitegemea Maswi angechukua fomu mapema kwa kuwa alionekana kukubalika zaidi, lakini kimya chake kikazidi kututia wasiwasi mpaka muda wa kuchukua fomu ukaisha jana bila kuchukua fomu hatujui tumuunge nani kati ya hao ambao majina yatarudi labda tutasubiria tuone yeye atamuunga nani kama ni Nyangwine na sisi tutaenda na huyo”, alisema mkazi mmoja wa Nyamongo aliyeomba jina lake lisitajwe.
Kuna wanaoamini kuwa kwakuwa Maswi hajachukua fomu basi kura kutoka maeneo anayopendwa zaidi zinaweza kuelekezwa kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo hilo, Nyambari Nyangwine au kwa mtiania ambaye watu hawamtarajii ambaye hasikiki sana kwa Wananchi na kwenye mitandao ya kijamii.
Wengine wanasema kura za Nyamongo zinaweza kwenda kwa Nicolaus Chichake, mzawa wa eneo hilo ambaye naye tayari ametia nia wengine wanasema huwenda akamuunga Dk Edward Machage hivyo kila mtu anatoa maoni yake kwa mtazamo wake lakini ukweli anao Maswi kwani bado yuko kimya.
Kwa sasa, mjadala mkubwa unaendelea ni juu ya ukimya wa Maswi wakisubiria waone hili jambo ambalo linaweza kubadili kabisa mwelekeo wa mchakato wa kura za maoni ndani ya chama husika.
Baadhi ya wananchi wanadai huwenda nafasi ya Nyambari Nyangwine inaweza kuimarika zaidi, lakini ushindani bado utabaki kuwa mkali hasa kwa kuwa uteuzi wa mwisho utafanywa na wajumbe wa chama kwa kuchuja majina matatu ya kupelekwa mbele kwa hatua zaidi na majina yaliyokuwa yakitajwa ni Eliakimu Maswi, Nyambari Nyangwine pamoja na Mwita Waitara haya ndiyo majina yaliyokuwa na nguvu zaidi.
Wananchi wengi wamesema watasubiri hadi mwisho wa mchakato hadi yatakaporudi majina matatu waone chaguo la Maswi ni nani na huyo ndiye watamuamini ambaye anaweza kuleta mabadiriko katika jimbo la Tarime vijijini.
Mwananchi mwingine ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe mkazi wa Magoto kijijini kwao Maswi, amesema amevunjika moyo kuona matarajio yake yamekwenda tofauti hivyo amekata tamaa ya kuendelea na duru za siasa.
Rhobi Mwita mkazi wa Borega kijiji jirani na Magoto yeye amesema kwa kuwa Maswi hagombei katika majina matatu yatakayorudi endapo jina la Nyambari Nyangwine litakuwemo, anatamani kuona anarudi kuwa Mbunge wa Tarime Vijijini.
Hata hivyo katibu wa Ccm Wilaya ya Tarime aliwambia waandishi wa habari kuwa waliojitokeza kuchukua fomu tangu Juni 28, 2025 toka Tarime vijijini ni watu 12 wanaume 10 na wanawake 2 wote walijaza fomu na kuzirejesha ambapo hadi kufikia Julai 2, 2025 saa 10 jioni walikuwa wamemaliza kuwasilisha fomu zao.