Na Josea Sinkala, Mbeya.
Wazazi na walezi katika kata ya Ilungu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya mkoani Mbeya, wameiomba Serikali ya Halmashauri ya Mbeya kushirikiana nao ili kuhakikisha shule yao ya sekondari ya Ilungu inajengewa uzio na bweni la watoto wa kiume ili kuongeza ulinzi na usalama kwa wanafunzi.
Wakizungumza na Jambo TV katika eneo la shule ya sekondari Ilungu, wazazi na walezi wanasema shule yao imefanya vizuri kitaaluma kwani imekuwa ya pili katika wilaya ya Mbeya lakini inakabiliwa na changamoto chache ambazo endapo zitakamilishwa itasaidia zaidi kuinua kiwango cha elimu shuleni hapo.
Wamewashukuru wadau wa elimu ambao ni wazawa wa kata ya Ilungu lakini wengi wakiishi nje ya kata ya Ilungu kwa kujitoa fedha na vitendea kazi kwa wanafunzi hasa waliofanya vizuri kitaalum katika shule hiyo ya sekondari na kuomba Serikali kuongeza matundu sita ya vyoo shuleni hapo, nyumba za watumishi, uzio wa shule na uboreshaji barabara kutoka kijijini Ifupa hadi shuleni Ilungu.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ilungu Ibrahim Mwakasege, amesema maendeleo ya kata yake lazima yaanze na wana Ilungu wenyewe hivyo kuwashukuru wadau kwa utayari wao na kuhusu uboreshaji miundombinu ya shule hiyo ameanzisha mchango kwa wananchi wake ili kuanza ujenzi wa matundu ya vyoo na kuwa anakwenda kuwasilisha maombi hayo Halmashauri kwa utatuzi zaidi wa maeneo yanayohitaji nguvu ya Halmashauri.

Afisa tarafa ya Tembela Odavia Webby, amewasilisha salamu za Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Beno Malisa akiwashukuru wananchi kwa kujitoa kwenye shughuli za maendeleo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuungana nao kuhakikisha changamoto ambazo bado hazijashughulikiwa zinatafutiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na mwendelezo wa kuboresha miundombinu ya shule ya sekondari Ilungu.

Odavia amesisitiza kuwa wakati Serikali inaendelea na uboreshaji miundombinu hiyo ya kielimu wazazi na walezi wakawekeza kwenye elimu kwa kuhakikisha hakuna mtoto anayepaswa kuwa shule anasalia uraiani kwa sababu yoyote.