Mbunge wa jimbo la Kibiti mkoa wa Pwani, Twaha Ally Mpembenwe ametoa wito kwa wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuacha kuuza maeneo kiholela kwa wafugaji wanaoingia katika maeneo hayo ili kuepusha migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika wilaya hiyo.
Kauli hiyo ameitoa Julai 11, 2024 katika Kijiji cha Rugungu kata ya Rualuke wakati akijibu kero za wanakijiji hao zilizohusu migogoro ya ardhi kati yao na wafugaji wanaodaiwa kuvavamia maeneo yao ya kilimo.
Mpembenwe amesema migogoro mingi imekuwa ikichangiwa na viongozi hao wa kijiji kutokana na kuuza maeneo bila utaratibu kwa wafugaji.
Sanjari na hayo Mpembenwe ameendelea kuwapa taarifa wapiga kura wake juu ya bajeti ya fedha ya mwaka 2024/25 katika Jimbo la Kibiti ambapo amesema imepita kwa asilimia zote hivyo wategemee fedha zote zilizoombwa katika bajeti yao ya maendeleo ya wilaya kuletwa zote kama zilivyoombwa.