Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Alhaji Juma Mkoma, amesema kuwa tathmini ya kina ya utendaji wa watumishi ni muhimu, ikijumuisha tabia na mienendo yao, ili kuhakikisha kuwa wanaopandishwa vyeo ni wale wenye maadili mema, na si kwa sababu ya muda waliokaa kazini pekee.
Akizungumza jijini Dodoma kwenye kikao cha kubadilishana uzoefu kuhusu maadili na utawala bora, Mkoma amesema “Tabia na mienendo ya watumishi lazima ifanyiwe tathmini, hatua hii itasaidia kuhakikisha kuwa wale wanaopandishwa vyeo ni wale walio na maadili mema na si kwa sababu tu wamefanya kazi kwa miaka mingi,”
Akiendelea na maelezo yake, Mkoma ameeleza kuwa watumishi wa umma wanapaswa kupewa mafunzo ya masuala ya maadili mara wanapoingia kazini, huku akisisitiza umuhimu wa kanuni za maadili ya utendaji kuwekwa wazi na kupatikana kwenye tovuti rasmi za ofisi husika.
Mbali na hayo Mkoma pia amesisitiza
umuhimu wa kuwa na mifumo thabiti ya ulinzi kwa watoa taarifa wanaoripoti vitendo vya ukiukwaji wa maadili sehemu za kazi nakudai mifumo hiyo inalenga kuwalinda watu wanaotoa taarifa ili wasidhurike.
Ameongeza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya watumishi watakaothibitika kukiuka maadili, hususan wanapojihusisha na vitendo vya rushwa na kusisitiza kwamba rushwa ni kosa la jinai na sheria itachukua mkondo wake.
“Sasa ili tufanikiwe kutatua changamoto kwenyeSuradili lazima tutumie TEHAMA, ni wazi kuwa matumizi ya TEHAMA yataondoa ulazima wa mikutano ya ana kwa ana kati ya mtoa huduma na muhitaji, hali itakayopunguza vitendo vya rushwa mahala pa kazi,” amesema Mkoma.
Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili katika Utumishi wa Umma, Leila Mavika amesema kikao hicho kililenga kuimarisha maadili na kuboresha mifumo ya utawala bora ili kupunguza mianya ya rushwa, nakuongeza kuwa maazimio matano yalipitishwa, yote yakiwa na lengo la kuboresha maadili na taaluma zaidi.
Kikao hicho kinalenga kutumia TEHAMA kama nyenzo muhimu ya kuboresha utendaji na utawala bora katika sekta ya umma, kwa lengo la kufikia ufanisi na uwazi zaidi.