Latest Posts

WANASAYANSI WA MAZINGIRA WAASWA KUTUMIA LUGHA RAHISI KWA JAMII

Wito umetolewa kwa wanasayansi wa mazingira kuhakikisha wanawasilisha tafiti zao kwa kutumia lugha rahisi na njia shirikishi kama hadithi, ili jamii iweze kuelewa kwa urahisi na kushiriki kikamilifu katika masuala ya uhifadhi jumuishi na endelevu.

Wito huo umetolewa Mei 3, 2025 katika mafunzo maalum ya siku tano kwa wanasayansi wa mazingira yaliyofanyika mkoani Mara, yakiandaliwa na Shirika la Grumeti Fund kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Leiden kutoka Uholanzi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mwezeshaji Ghaamid Abdulbasat amesema kwa muda mrefu wanasayansi wamekuwa wakibadilishana taarifa baina yao pekee kwa kutumia lugha ngumu, hali inayosababisha jamii kushindwa kushiriki ipasavyo katika masuala ya uhifadhi.

“Ili kuleta mabadiliko ya kweli, lazima tuzungumze kwa njia ambazo umma unaweza kuhusiana nazo. Sayansi isiyowasilishwa kwa jamii haijafika,” alisema Abdulbasat.

Alieleza kuwa mawasiliano ya sayansi ni muhimu kwa ajili ya kushawishi sera na kuongeza uelewa wa umma, jambo ambalo linaimarisha utekelezaji wa tafiti kwa vitendo katika jamii husika.

 

Janeth Mgure, mwanafunzi wa shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na mwanzilishi mwenza wa Shirika la Human-Wildlife Co-existence Foundation, amesema mafunzo hayo yamewapa uelewa mpya juu ya umuhimu wa kutumia lugha nyepesi na inayoeleweka.

“Wasomi wengi tumekuwa tukitumia lugha ngumu pasipo kujua kama ujumbe unawafikia walengwa. Haya mafunzo yametufungua macho na mioyo,” alisema Mgure.

Aliongeza kuwa pengo la mawasiliano kati ya wanasayansi na jamii limekuwa changamoto kubwa katika utekelezaji wa tafiti nyingi nchini, lakini kupitia ujuzi walioupata, wapo tayari kulifunga pengo hilo.

Victoria Mkesa, Mratibu wa Programu ya Utafiti na Ubunifu (RISE) kutoka Grumeti Fund, alisema mafunzo hayo yamekusudiwa kuwawezesha wanasayansi hao kufikisha tafiti zao kwa njia zinazogusa maisha ya watu, hasa kwa kutumia hadithi kama zana ya mawasiliano.

“Tunajua mazingira yanahusiana moja kwa moja na maisha, ardhi na historia ya watu wetu. Ndiyo maana tunasisitiza matumizi ya hadithi, kwa kuwa ni lugha ya moyo ambayo jamii inaweza kuelewa kirahisi na kuichukulia hatua,” alisema Mkesa.

Alisema washiriki 10 kutoka taasisi mbalimbali nchini walipata ujuzi wa namna ya kubadili taarifa ngumu za kisayansi kuwa maudhui ya kueleweka kwa jamii, hivyo kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika uhifadhi wa mazingira.

 

Kwa ujumla, mafunzo hayo yameelezwa kuwa chachu ya mabadiliko katika namna ambavyo watafiti wa mazingira wanapaswa kuwasiliana na jamii, ili kuhakikisha sayansi haibaki kwenye makaratasi bali inakuwa sehemu ya maisha halisi ya watu.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!