Na Josea Sinkala, Mbeya.
Kampeni ya mama Samia Legal Aid inayohusu utoaji ushauri wa masuala ya kisheria, migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi imetembelea na kufanya mkutano wa hadhara katika kijiji na kata ya Ifumbo wilayani humo na kuelimisha masuala mbalimbali yahusuyo masuala ya kisheria.
Mratibu wa kampeni ya Samia Legal Aid wilaya ya Chunya ambaye pia ni wakili kutoka Wizara ya katiba na sheria bi. Judith Kapaga, ameambatana na viongozi wengine mbalimbali katika wilaya ya Chunya kwenda kutoa elimu katika kijiji cha Ifumbo na kwa watoto wa shule ya upili Ifumbo waliofundishwa mambo mbalimbali ikiwemo kutambua viashiria vya ukatili na kuzingatia masomo.
Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, afisa ustawi wa jamii wilaya ya Chunya Lutness Mbisa, amesema ukatili wa kijinsia, migogoro katika ndoa na unyanyasaji bado vinaendelea kushuhudiwa miongoni mwa wana ndoa jambo linalozorotesha upendo na kurudisha nyuma ustawi wa familia.
Amesema kinachoshangaza ni kuona baadhi ya wana ndoa wakike wakiwatoza waume zao fedha ili kushiriki tendo la ndoa.
“Akina baba niwaulize vipi ile ibada ya usiku ipo? Akina mama vipi ile ibada mnapata? Huko tulikotoka maana tumepita kata 19 hii ni kata ya 20 tumeambiwa wanaume hawapewi hiyo ibada (tendo la ndoa) hadi walipie na tulipowauliza wanawake kwanini muwatoze waume zenu wakasema ni kwasababu huko nje (kwenye michepuko) wanashiriki na kutoa hela sasa utaona tunavyoishi lakini ukweli haitakiwi kuwa hivyo na imefikia mahali sisi wazazi hadi watoto wadogo hawa vijana wameanza kuolewa na mashangazi (wanawake watu wazima) shida ni malezi kwetu wazazi maana hawa watoto hawakudondoka tu bali muunganiko wetu wazazi ndio ulileta watoto”, ameeleza afisa ustawi wa jamii wilaya ya Chunya Lutness Mbisa.
Kwa upande wake ndugu Moli Masoud ambaye ni afisa ardhi kutoka ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Chunya, amewataka wananchi kufahamu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za umiliki wa ardhi ili kuepuka migogoro inayoepukika huku wananchi wakihimimizwa pia kuzingatia umuhimu wa kuandika wosia badala ya kuwa na dhana kwamba kuandaa wosia ni kujitabiria kifo.
Baadhi ya wananchi waliozungumzia mafunzo hayo wmaeomba elimu hiyo kuwa endelevu kwani imewafungua kwa sehemu kubwa kutambua masuala mbalimbali hasa kwenye ndoa zao na umilikaji ardhi katika kuepuka matatizo yanayoepukika na kufikia maendeleo endelevu.
Kambi ya wasaidizi wa kisheria kupitia timu ya mama Samia legal Aid pamoja na wilaya nyingine na maeneo mengine nchini pia imeweka kambi wilayani Chunya kwa kutembelea maeneo na wananchi mbalimbali kwa ajili ya kutoa elimu ya masuala ya kisheria, migogoro ya ardhi, mirathi na ndoa wakielekeza zaidi ushauri wao katika kuwasaidia wananchi kuepukana na migogoro mbalimbali na kujikita kwenye shughuli ya kimaendeleo.