utokana na ongezeko la matukio ya ukatili wa kijinsia nchini, Taasisi ya Foundation For Disabilities Hope (FDH) imeanza kutekeleza mradi wa kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu. Mradi huu unalenga kutoa elimu na kuwajengea uwezo wanawake na watoto wenye ulemavu ili waweze kujua haki zao za msingi na kuripoti matukio ya ukatili.
Akizungumza wilayani Chamwino, wakati wa mafunzo kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili, Mratibu wa mradi huo, Glory Mbowe, alisema lengo kuu la mradi ni kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wenye ulemavu. Pia, alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu juu ya haki za binadamu ili kundi hilo maalum litambue haki zao.
“Mradi huu unalenga kuwajengea uwezo wanawake na watoto wenye ulemavu ili waweze kutambua haki zao na kuripoti vitendo vya ukatili kwa vyombo husika. Hii itawasaidia kukabiliana na changamoto za ukatili wanazokutana nazo,” alisema Mbowe.
Mafunzo hayo, yanayotekelezwa katika Kata ya Buigiri wilayani Chamwino, pia yamekuwa na lengo la kuwafundisha watu wenye ulemavu namna ya kujilinda dhidi ya ukatili. Mbowe alibainisha kuwa mafunzo haya yataongeza uelewa miongoni mwa wanawake na watoto wenye ulemavu ili waweze kuchukua hatua pale wanapokumbana na vitendo vya ukatili.
Mwezeshaji kutoka Dawati la Jinsia la Kituo cha Polisi Chamwino, Malale Michael, alieleza kuwa mafunzo hayo yamejikita zaidi katika kuwafundisha washiriki maana ya ukatili na aina zake, pamoja na jinsi ya kutoa taarifa za vitendo hivyo. “Tunawaelimisha namna ya kutambua ukatili ni nini, aina zake, na jinsi ya kutoa taarifa ili vyombo vya dola viweze kuchukua hatua stahiki,” alisema Michael.
Aidha, alieleza kuwa Wilaya ya Chamwino bado inakabiliwa na matukio ya ukatili, ikiwemo ndoa za utotoni, ulawiti, na ubakaji, ingawa hali si mbaya sana. Jeshi la Polisi limeanzisha kampeni ya kuzuia vitendo vya ukatili yenye kauli mbiu, “Tuchukue hatua kabla hawajaharibiwa,” alisema Malale.
Pia, jeshi hilo limekuwa likitoa elimu kupitia nyumba za ibada, likiwalenga wananchi ili kuwaongezea uelewa kuhusu vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wenye ulemavu.
Mwanasheria wa FDH, Joyce Mhana, alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kila binadamu ni sawa, na hakuna sababu yoyote inayompa mtu haki ya kumfanyia mwenzake ukatili. Aliongeza kuwa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 inamtaka kila mtu kuwalinda watu wenye ulemavu, na kushindwa kufanya hivyo kunachukuliwa kama kushiriki katika ukatili huo.