Zaidi ya wanawake 100 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara wanatarajiwa kupata mafunzo maalumu kuhusu ushiriki wao katika nafasi mbalimbali za uongozi kuelekea uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba 2024, na uchaguzi mkuu mwaka 2025.
Hayo yalibainishwa Septemba 3, 2024, wakati wa uzinduzi wa mradi wa Mwanamke Sasa, unaotekelezwa na Shirika lisilo la kiserikali la FB-Empowerment, lenye makao yake mkoani Mtwara, ulifanyika katika ofisi za halmashauri hiyo.
Mratibu wa mradi, Shakila Hamisi alieleza kuwa lengo kuu la mradi huo ni kuongeza idadi ya wanawake wanaowania nafasi za uongozi kutokana na idadi ndogo ya wanawake viongozi katika halmashauri hiyo.
“Mtwara Vijijini ina jumla ya vijiji 110, lakini wenyeviti wa vijiji wanawake ni wawili tu. Hivyo, tumeona kuna haja ya kuwajengea uwezo wanawake na mabinti wenye umri wa kuanzia miaka 18, ili wawe na uthubutu na ujasiri wa kuwania nafasi za uongozi. Lengo letu ni kuona tunapata angalau wanawake 50 katika nafasi hizo, ikilinganishwa na idadi ya wawili waliopo sasa”, ameeleza Shakila Hamisi.
Katika uzinduzi huo, Diwani wa Kata ya Ndumbwe, Mahupa Abdul alitoa wito kwa shirika hilo kuhakikisha wanawaondoa wanawake katika imani potofu ya kudhani kuwa kila mgombea au kiongozi lazima awe mshirikina.
“Ushirikina ni jambo ambalo linaathiri na kudumaza jamii yetu, na ni muhimu wanawake wajue kuwa uongozi bila ushirikina unawezekana kabisa,” alisema Mahupa.
Kwa upande wake, Alfred Mtawali aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, alisisitiza umuhimu wa viongozi kuhamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika mradi huo.
“Ningependa kutoa angalizo kwa wananchi wetu. Huu mradi ni wa kwetu, na ni muhimu sisi viongozi, hususan kina mama, kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu ili waweze kuwa chanzo cha mafanikio,” alisema Mtawali.
Katika hotuba yake, Winfrida Linyembe, Afisa Tarafa wa Tarafa ya Ziwani, aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara aliitaka taasisi hiyo ya FB-Empowerment kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa inawahusisha pia wanaume ili waweze kuwa mabalozi wazuri katika kuisemea taasisi hiyo na kuchangia mabadiliko chanya katika jamii.
Mradi wa Mwanamke Sasa unatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi sita, kuanzia Agosti 2024 hadi Januari 2025. Kwa hatua za awali, mradi huo unatekelezwa katika kata tatu za halmashauri hiyo, ambazo ni Nanguruwe, Kitere, na Msangamkuu, ambapo kila kata itawashirikisha wanawake 40 katika mafunzo hayo.
Mradi huu wa Mwanamke Sasa unatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa katika ushiriki wa wanawake katika uongozi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, na hivyo kuwa mfano mzuri kwa maeneo mengine nchini.