Latest Posts

WANNE WAKAMATWA WAKITUHUMIWA KWA MAUAJI YA AFISA WA TRA, DAR ES SALAAM

Na; mwandishi wetu

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watuhumiwa wanne (4) huku wengine wakiendelea kuhojiwa kwa kina, wakidaiwa kufanya mauaji ya mtumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) aitwaye Amani Kamguna Simbayao

Kamanda wa Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Jumanne Muliro ameeleza hayo alipokutana na wanahabari, Jumamosi Desemba 07.2024 ambapo amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Deogratius Paul Massawe (40) ambaye ni kuli mkazi wa Tegeta, Bakari Idd Bakari (30) kuli mkazi wa Tegeta kwa Ndevu, Omar Issa, Myao ambaye ni mpiga debe wa Tegeta Dawasco, na Rashidi Mtonga, Myao (29) dereva bodaboda.

Katika mkutano huo wa wanahabari uliofanyika Central Police, jijini Dar es Salaam SACP Muliro pia amesema watuhumiwa hao wamemjeruhi mtumishi mwingine wa TRA aliyefahamika kwa jina la Adriano Fredrick

“Watuhumiwa hao ambao bado wanahojiwa kwa kina wakati wakiwashambulia maafisa hao waliliharibu pia gari la serikali la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) lenye namba STL 9923 aina ya Toyota Land cruizer had top nyeupe mali ya TRA” -SACP Muliro

SACP Muliro amesema tukio hilo limetokea Desemba 05.2024 majira ya saa 3 usiku eneo la Tegeta kwa Ndevu, Kinondoni, jijini Dar es Salaam, ambapo tukio hilo lilitokea baada ya maafisa hao wa TRA kukamata gari lenye namba T529 DHZ aina ya BMW rangi nyeupe ambalo lilidaiwa kuwa na makosa ya kikodi

“Wakati wakitekeleza majukumu hayo ya kisheria, maafisa hawa wa TRA licha ya kufuata taratibu za kisheria lilijitokeza kundi la watu wakiwemo hao ambao nimewataja walianza kuwashambulia kwa mawe, kuliharibu gari la TRA yaani la serikali, na baadaye kusababisha kifo cha mtumishi huyo wa serikali ambaye nimemtaja” -SACP Muliro

Aidha, Jeshi hilo limetoa onyo kali na kwamba halitavumilia watu ambao wanataka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa serikali wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisheria, kwa kuwa licha ya kuwa watumishi hao wanazifuata taratibu za kiutendaji lakini bado kuna tabia inayotaka kujengeka ya watu kutaka kuwashambulia watumishi wa serikali kwa sababu mbalimbali ambazo hazikubaliki

“Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es Salaam halitasita kuchukua hatua kali za kisheria na za haraka dhidi ya wahusika ikiwa ni pamoja na kuwahoji, kuwakamata na kuwapeleka kwenye mamlaka zingine za kutenda haki” -SACP Muliro

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!