Latest Posts

WAPAMBE WA SERIKALI MSITUFANYE WANANCHI HATUNA AKILI, SHIDA SIYO MAADILI KWENYE (X) TWITTER

Na John Marwa.

Takribani wiki moja sasa kumekuwepo na kampeni ama vuguvugu linaloendeshwa na makundi mbalimbali nchini ikiwemo viongozi wa dini, vyama vya siasa na hatimaye jana, Jumanne Juni 11.2024 UVCCM walitoka hadharani na kuitaka serikali kupiga marufuku ama kuufungia mtandao wa ‘X’ zamani ukijulikana kama ‘twitter’ kwa kile walichodai kuwa mtandao huo umeanzisha sera ambayo inaruhusu kupakia ama kutazama maudhui ya mapenzi ya jinsia moja kwa maana ya kuchochea vitendo vya ushoga na usagaji

Vikundi hivyo ambavyo ukivitazama kwa uhalisia ni vikundi ambavyo ni wapambe wa serikali/ watawala vimejikita katika hoja ya kwamba serikali inapaswa kuchukua hatua hizo ili kulinda kile wanachokiita maadili ya Tanzania na kuwalinda raia wake dhidi ya wimbi kubwa ambalo Dunia inakumbana nalo kwa sasa la mapenzi ya jinsia moja

Kwa bahati mbaya ama nzuri vikundi vinavyoshinikiza jambo hilo vimeshindwa kujipanga kwa hoja ama aliyewatuma ameshindwa kuwapa darasa ama hoja madhubuti kitendo kinachopelekea umma wa Watanzania kuvinyooshea kidole kila kona kwa namna ambavyo vikundi hivyo vinaratibu hili vuguvugu kiasi kwamba wadadisi wa mambo nikiwemo mimi kufikia hitimisho kwamba kuna mtu ama taasisi imewatuma hawa UVCCM, viongozi wa dini na wengineo ili kuja kupima upepo baada ya kuona mtandao huo wa ‘X’ (twitter) umekuwa mwiba mkali kwa watawala kwani sehemu kubwa ya watumiaji wa mtandao huo wamekuwa wakihoji, kukosoa na wakati mwingine kwa lugha kali kila sera, maamuzi na mienendo ya serikali kiasi kwamba kuelekea chaguzi zijazo (uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu mwakani) joto la kisiasa jisni linavyozidi kupanda, wameona hawana uwezo wa kuvumilia mishale inayotoka kwenye mtandao huo, hivyo kufikiria njia pekee ya kujinasua kwenye kadhia hiyo ya ukosoajini kuufuta mtandao huo kwenye anga la Tanzania.

Unaweza kujiuliza je, ni kweli mtandao wa ‘X’ (twitter) unaruhusu maudhui ya ngono au maudhui ya jinsia moja?, mwandishi wa makala hii nafahamu kwamba ni ukweli usiopingika kuwa mtandao wa ‘X’ (twitter) kama ambavyo mitandao mingine yote Tanzania na Duniani inaruhusu watumiaji kupakia maudhui ya ngono kama mtumiaji atataka, mfano kwenye ‘X’ (twitter) kuna kitu kinachoitwa ‘Algorithms’ ambacho kinaruhusu wewe mtumiaji wa mtandao huo kuletewa kwenye timeline yako aina ya maudhui unayoyatafuta ama ambayo uko na hamasa nayo, kama hujakuwa interested na maudhui ya ngono huwezi kuyaona kwenye timeline yako.

Sasa kinachonishangaza hapa ni kwamba hao UVCCM na wenzao Masheikh wameenda kwenye ‘X’ (twitter) wametafuta maudhui ya ngono, wametazama vyema halafu wanakuja kuleta ngonjera zao kwamba mtandao huu ufutwe?, watuambie hawa watu wamefikaje kwenye maudhui ya ngono?, wamefuata nini kwenye hizo timelines zenye kubeba hayo ‘mapilau’?, maana mtandao huu wa ‘X’ (twitter) unakuletea kitu ambacho umekiulizia wewe mtumiaji, sasa hawa kama wanakerwa na maudhui ya ngono wamefikaje huko?.

Maswali mengine ya kujiuliza, kwa nini mtandao wa ‘X’ (twitter) tu ndio wameushikia bango?, hawa watu wanafahamu kweli kwamba kuna mtandao unaitwa TikTok?, wanafahamu ‘ushetani’ unaofanyika huko TikTok?, wanafahamu kweli watoto wadogo kabisa wanavyojiuza, kusagana na mambo ya ushoga yanayoendelea huko TikTok?, jibu ni kwamba wanafahamu vyema lakini kwa sababu mtandao huo wa TikTok hakuna serikali ama watawala kuhojiwa huko, basi hawana ugomvi nao.

Mfano mwingine tena wa wazi ni kuhusu mtandao wa Clubhouse, mtandao huu umefungwa katika anga la Tanzania kwa muda mrefu sana, je kuliwahi kupakiwa maudhui ya ngono ama ya mapenzi ya jinsia moja huko Clubhouse?, mtandao huu ndio ulikuwa tishio namba moja kwa watawala maana hoja za ukosoaji zilikuwa zinabandikwa na mijadala kuhusu maswala mbalimbali ya kisiasa ilikuwa ikiendeshwa huko usiku na mchana hadi hapo wenye mamlaka/ serikali waliposhindwa kuvumilia aina ile ya ukosoaji wakaufungia, na hapakuwahi kuwa na picha ama video yoyote ile ya ngono achilia mbali mapenzi ya jinsia moja kuwa sehemu ya maudhui ya mtandao huo, kwa hiyo watu wenye akili timamu hawawezi kuingia kwenye mtego huu wa wapambe hawa kutaka kuzuia sauti za wananchi kuhoji watu waliopewa dhamana kwa kigezo cha kulinda maadili ambayo kwanza hayapo.

Kama kweli UVCCM na Masheikh wanakerwa na ushoga na usagaji mbona kila kona hususani kwenye jiji la Dar es Salaam haya mambo yameshageuka kuwa utamaduni?, leo ‘X’ (twitter) ndio ije kubebeshwa lawama za ushoga?.

Jambo jingine ambalo lilinishtua hadi kuandika makala hii, ni kwa nini uratibu wa mikutano hii ya UVCCM na wanahabari pamoja na ile ya Masheikh na wanahabari ifanane kwa kila kitu?, kwamba ilikuwa ni kwa bahati mbaya?, yaani aliyewaita waandishi wa habari wakafanye coverage kwa Mwenyekiti wa UVCCM ndio huyohuyo aliyeratibu mkutano wa waandishi wa habari wa Masheikh kuzungumzia mada hiyohiyo na maudhui yao ni yaleyale.

Mimi kama Mwanahabari ninaitahadharisha serikali kwamba ijitenge na hili jambo kwani hasira za wananchi ziko wazi kwenye hili sakata, iepuke haya magenge ya wapambe kwa sababu sina imani kwamba kweli serikali inashindwa kukabiliana kwa hoja na wakosoaji wake.

John Marwa ni Mkurugenzi wa JAMBO TELEVISION ONLINE,
0767252999.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!