Waratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mkoani Kigoma wametakiwa kuwajengea uwezo wanufaika wa mradi huo ili waweze kufuzu na kuweza kujitegemea kiuchumi kwa lengo la kuachana na utegemezi wa mfuko huo kuendesha maisha yao.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye alipozungumza wakati akifungua kikao kazi cha viongozi wa mkoa na wilaya kilichofanyika mjini Kasulu na kusisitiza kuwa wanufaika wanapaswa kutumia fedha wanazopata kuibua miradi itakayowafanya waweze kujitegemea.
Amesema wanufaika wanapofikia hatua ya kujitegemea wanatoa fursa kwa walengwa wapya au waliokosa nafasi katika mpango wa awali hali inayosaidia kuongeza idadi ya wananchi watakaoguswa na huduma za mradi huo.
Ameeleza kuwa sambamba na kuzidi kuwajengea uwezo wanufaika, wanapaswa kupiga hatua zaidi kwa kuijengea jamii uelewa chanya kuhusu utekelezaji wa mradi huo kwa kutoa taarifa za hatua na maendeleo yanayofikiwa.
Amesema kikao hicho kitasaidia kuwajengea uelewa viongozi wa serikali ili waweze kuwa na majibu pale ambapo jamii inahitaji kupata ufafanuzi kuhusu hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi.
“Kikao hiki kitatupa dira mpya na kuwezesha kila mmoja wetu kuwa mwalimu na kuweza kutatua changamoto wanazokutana nazo wananchi kuhusu hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi” Amesema Andengenye.