Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Taifa, Tundu Lissu, ameweka wazi kuwa yuko tayari kuwapokea wabunge 19 wa viti maalum waliodaiwa kuingia bungeni bila baraka za chama, lakini akasisitiza umuhimu wa uwazi na uwajibikaji kwa hatua yao ya kurejea.
Lissu ametoa kauli hiyo wakati wa mahojiano na kituo cha habari cha Bongo FM siku ya Ijumaa, Januari 24, 2025, ambapo ameonesha mashaka juu ya uhalali wa mchakato uliowawezesha wabunge hao kufika bungeni, akidai kuwa kuna maswali mengi yasiyojibiwa kuhusu hatua hiyo.
“Nipo tayari kuwapokea kina Halima Mdee na wenzake, lakini nina shida nao sana. Watu ambao waliingiaje Bungeni? Hawajawahi kusema hizo fomu za kugombea nani aliyewapa? Nani aliyezisaini? Nani wa CHADEMA aliyezisaini, kwasababu Katibu Mkuu Mnyika hakuwahi kusaini hizo fomu, na sheria ya chama inasema lazima zisainiwe na Katibu Mkuu,” amesema.
Lissu amesisitiza kuwa wabunge hao wanapaswa kueleza hadharani mchakato wa wao kuingia bungeni, akitilia shaka usahihi wa hatua hiyo. Ametoa mfano wa Nusrath Hanje, mmoja wa wabunge hao, ambaye alikamatwa na kuwekwa gerezani lakini baadaye alionekana bungeni kama mbunge wa viti maalum.
“Huyo aliyekuwa gerezani, ilikuaje akatoka gerezani akaenda kuapa kuwa mbunge? Nani aliyemfuata gerezani kumpa habari njema hizi?” amehoji.
Kwa mujibu wa Lissu, hatua ya wabunge hao kurudi CHADEMA inapaswa kuwa na dhamira ya kweli ya kutafuta suluhu, siyo kwa sababu uchaguzi mkuu unakaribia na wanatafuta kuhalalisha nafasi zao za ubunge. Lissu ameweka bayana kuwa kurejea kwa wabunge hao kunapaswa kuambatana na uwazi wa nia na mchakato wa kweli wa kujenga chama.
“Kama wanarudi CHADEMA, waje wafungue siri za mioyo yao. Wanataka suluhu na chama, waje wakiwa na mioyo myeupe na tuichunguze ni myeupe kweli. Wasije tu kwasababu uchaguzi umekaribia, wakitaka waendelee kuwa wabunge,” ameongeza.