Latest Posts

WASIRA AZINDUA KAMPENI ZA CCM IRINGA MJINI, AWASHAURI WANANCHI KUCHAGUA CHAMA HICHO KWA MAENDELEO

Na Mwajuma Hassan , Iringa

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amezindua rasmi kampeni za uchaguzi katika Jimbo la Iringa Mjini na kuwataka wananchi kuendelea kukichagua CCM kwa ajili ya kuwaletea maendeleo na kudumisha amani ya nchi.

Uzinduzi huo umefanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa, Manispaa ya Iringa, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho akiwemo Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (MCC) Salim Abri, pamoja na maelfu ya wananchi.

Akihutubia wananchi, Wasira alisema kuwa CCM ni mwendelezo wa mapambano ya uhuru, uchumi na ustawi wa jamii, akisisitiza kuwa chama hicho kina rekodi ya utekelezaji wa ilani zake tofauti na vyama vingine ambavyo, kwa kauli yake, havina historia ya kutekeleza.

Katika kuelezea vipaumbele vya Ilani ya CCM ya mwaka 2025–2030, Wasira alitaja mipango ya kujenga shule 22 za msingi na sekondari, kuanzisha vituo vya afya 7 na zahanati 15, kuongeza huduma za kijamii, pamoja na kuboresha sekta ya kilimo kupitia ruzuku kwa wakulima, usambazaji wa mbolea kwa wakati, na kuanzisha vituo vya zana za kilimo na ufugaji.

Aidha, alimkabidhi mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, nakala ya Ilani ya CCM ya kitaifa na ya mkoa ili aweze kufahamu kikamilifu mpango wa maendeleo wa jimbo hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, alisema kuwa serikali ya awamu ya sita imetekeleza miradi mikubwa ya maendeleo hususan katika sekta za maji, nishati, barabara na afya, jambo linaloonesha dhamira ya chama hicho katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.

Naye mgombea ubunge jimbo la Iringa mjini  Fadhili Ngajilo, ameahidi kushirikiana na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha miundombinu ya mitaa yote kwa kiwango cha lami. Alibainisha pia kuwa Iringa ina fursa kubwa za kiuchumi zinazohitaji kuendelezwa kwa ubunifu.

Ngajilo alimshukuru Rais Samia kwa kuahidi ujenzi wa Machinga Complex ili kusaidia wafanyabiashara wadogo, akisema kuwa utekelezaji wa miradi hiyo ni kielelezo cha dhamira ya CCM.

Ameongeza kuwa ifikapo Oktoba 29, wananchi wa Iringa Mjini watakipa kura CCM kwa kishindo, kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais, kwa kuwa chama hicho kina dira, sera na utekelezaji unaogusa maisha ya wananchi wa kawaida.

 

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!