Baada ya waandaaji wa tamasha la muziki wa kizazi kipya la Wasafi Festival ambao ni lebo ya muziki ya Wasafi kwa kushirikiana na Wasafi media (Wasafi FM na Wasafi TV) kutangaza kuhairisha kwa tamasha lililotarajiwa kufanyika Jumamosi hii ya Septemba 21.2024 uwanja wa CCM Nangwa Sijaona, mkoani Mtwara mjadala mpana miongoni mwa wadau umeibuka huku kila mmoja akiwa na mtazamo wake
Katika mapokeo ya kuhairishwa huko, wako wanaoamini kuwa huenda waandaaji wamekosa au wameishiwa fedha za kufanyia maandalizi, wapo wanaodai kuwa huenda mapokeo ya wakazi wa Mtwara yamekuwa finyu yaani huenda wakawa wamesuasua kukata tiketi hali iliyowalazimu waandaaji kuhairisha, wapo wengine waliogusia jambo hilo pengine na ‘vita’ ya kisanaa inayoendelea baina ya wasanii Diamond na Harmonize ikizingatiwa kuwa Mtwara ni nyumbani anakotoka Harmonize nk, kila mmoja amekuwa na mapokeo yake, na hii yote ikitokana na ukweli kwamba tangazo la kuhairishwa kwa tamasha hilo halijaambatanisha sababu za msingi za kuhairishwa kwake
Taarifa zilizopo ni kwamba hadi tamasha hilo linaahirishwa tayari hasara ya mamilioni ya fedha imeingiwa kutoka kwa waandaaji, wananchi wa kawaida hadi serikalini kwa kuwa mzunguko wa fedha uliotarajiwa ungewezesha hadi serikali kukusanya mapato
Ukweli ni kwamba uwepo wa matamasha ya aina hiyo umekuwa ukichochea uchumi wa eneo husika na Taifa kwa ujumla wake kwani mnyororo wa thamani ya fedha unaweza kumnufaisha kuanzia mama/ baba lishe, Bodaboda, wamiliki wa nyumba za kulala wageni (Guest House, Lodge, Hotels nk), wafanyabishara wadogo kwa wakubwa nk, lakini kuhairishwa kwake maana yake makundi hayo yote sasa badala ya kunufaika na uwepo wa tamasha hilo sasa imekuwa kinyume chake kwa kuwa yameingia hasara kwa namna moja au nyingine, huku hasara kubwa ikitajwa kuingiwa na waandaaji
Taarifa tulizonazo zinadai kuwa baadhi ya wasanii waliotakiwa kutumbuiza kwenye tamasha hilo walipaswa kusafiri leo, Ijumaa Septemba 20.2024 kwa ndege kutoka Dar es Salaam kuelekea Mtwara huku baadhi yao wakiwa wameshalipwa nusu ya malipo wanayostahili kulipwa, mmiliki wa uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona ambaye ni Chama cha Mapinduzi (CCM) naye ameshalipwa sehemu ya fedha anazotakiwa kulipwa, kama hiyo haitoshi Hotels zilizokuwa zimeshikiliwa kwa ajili ya kulala wageni pasi na shaka zinapaswa kulipiwa zote bila kujali zimetumika au la, hapo hujazungumzia maandalizi yaliyokuwa yanaendelea kwenye uwanja wa CCM Nangwanda Sijaona ambapo majukwaa ya tamasha hilo yalishatengezwa na sasa yanapaswa kubomolewa upya, sijasahau
Katika muktadha huohuo pia huwezi kusahau makampuni na taasisi zilizodhamini tamasha hilo ambazo pia tunazo taarifa kuwa tayari zilishaweka kambi Mtwara kwa muda sasa, na walishafunga matangazo/ mabango yao uwanjani hapo, huku kampuni za Wasafi media na lebo ya Wasafi pia nayo ikipeleka wafanyakazi wake mapema kabisa kwa ajili ya kusimamia kuhakikisha kila kitu kinaenda kama kilivyopangwa, hizo zote ni hasara ambazo zimetokea kwa kuhairishwa kwa tamasha hilo
Kupitia mitandao ya kijamii ya Wasafi media (Wasafi FM na Wasafi TV) waandaaji wamechapisha ujumbe unaosomeka ifuatavyo, “kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wetu tamasha la Wasafi Festival 2024 lililopangwa kufanyika Mtwara Septemba 21 (Nangwanda Sijaona) halitaweza kufanyika tarehe husika; na kwa sababu ya upendo mkubwa na mapokezi makubwa ambayo wana Mtwara mmekuwa mkituonesha siku zote tunaahidi tutarejea na kuwaletea msimu huu mkubwa wa burudani wa Taifa”, ujumbe huo umeambatanishwa na bango lililokuwa linatangaza uwepo wa tamasha hilo ambalo kwa sasa juu ya bango hilo kuna maneno yanayosomeka “Postponed”
Jambo TV tumelazimika kuingia chimbo ili kujuwa undani wa jambo hilo na kile kilichopelekea tamasha hilo kuhairishwa kwake, ambapo kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika kutoka mkoani Mtwara kimedai kuwa sababu za kuhairishwa kwa tamasha hilo kunakuja kufuatia vyombo vya ulinzi na usalama mkoani humo hususani Jeshi la Polisi kuwaeleza waandaaji kuwa tamasha hilo haliwezi kufanyika kutokana na wasiwasi wa kiusalama
Inadaiwa kuwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara limewaeleza waandaaji wa tamasha hilo kuwa kwa sasa wanaweza kupeleka tamasha hilo kwenye mikoa mingine na kwamba watapatiwa taarifa siku zake pindi vyombo vya ulinzi na usalama vitakapoona mambo yako sawa,
Ingawa haijafahamika moja kwa moja undani wa sababu hizo za kiusalama lakini inatakumbukwa kuwa mkoa huo unapakana na jimbo lenye utajiri wa mafuta, gesi na madini la Cabo Delgado la nchini Msumbiji, jimbo ambalo kwa muda mrefu sasa hali ya usalama iko shakani kutokana na kukabiliwa na makundi ya kigaidi ambayo wakati fulani inatajwa yaliwahi kuvuka mpaka na kufanya uharibifu kwenye baadhi ya vijiji vya Tanzania vilivyopo mpakani kabla ya kudhibitiwa
Chanzo hicho cha kuaminika hata hivyo kimetueleza kuwa Jeshi la Polisi halijawafafanulia waandaaji wa tamasha hilo kuwa wasiwasi wa kiusalama unaozungumzwa ni wa muktadha upi, ingawa inadaiwa moja ya maelekezo waliyopatiwa waandaaji wa tamasha hilo ni kutoa taarifa kwa umma kuwa wamesitisha tamasha hilo kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao kama walivyofanya,
Aidha, wapo wanadhani kuwa huenda kwa sasa Jeshi la Polisi liko kwenye mkakati kabambe wa kuzuia mikusanyiko inayobeba idadi kubwa ya watu ikizingatiwa kuwa kwa sasa wako kwenye maandalizi ya kukabiliana na watu watakaojitokeza kwenye maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambayo kimsingi wameyapiga marufuku
Katika upande mwingine unaweza usikubaliane na wale wanaotoa hoja hiyo kwa kuwa tamasha la Wasafi Festival lilitarajiwa kufanyika Septemba 21.2024, mkoani Mtwara lakini maandamano ya CHADEMA yanatarajiwa kufanyika Septemba 23.2024 jijini Dar es Salaam
Katika kutafuta kile kilichopo nyuma ya pazia ya jambo hilo, Jambo TV imezungumza kwa njia ya simu na Mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdallah Mwaipaya ambaye itakumbukwa kuwa mamlaka ya uteuzi imetangaza kumuhamishia wilayani humo hivi karibuni akitokea wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro
Katika mazungumzo yake Mwaipaya amedai kuwa kwa sasa yuko wilayani Mwanga akijiandaa kuelekea Mtwara, ni kwamba baada ya kuhamishiwa Mtwara alienda moja kwa moja kwenye kituo chake kipya cha kazi kwa ajili ya kukabidhiwa ofisi, lakini baadaye alirejea Mwanga ili naye akakabidhi ofisi jambo ambalo amelifanya, na kwamba kwa sasa anatarajiwa kurejea tena Mtwara kuendelea na kazi
Kuhusu uwepo wa taarifa hizo, na madai ya vyombo vya ulinzi na usalama Mtwara kuzuia kufanyika kwa tamasha hilo Mwanga amesema hajuwi chochote kwa kuwa hayuko ofisini kwa sasa, ingawa alipata taarifa kwa ufupi kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuwa Diamond na wenzake watafanya tamasha Mtwara lakini hakufahamu kwa kina tamasha hilo linahusiana na nini, na hata hakujuwa linafanyika lini
Mkuu wa wilaya huyo ameendelea kusisitiza kuwa kwa kuwa sasa ndo anaelekea kwenda kuanza kazi rasmi anaamini kama hilo lipo atapata taarifa pindi atakapofika ofisini sambamba na kuahidi kuendelea kufuatilia ili kujuwa undani wake
Jambo TV bado inaendelea kufuatilia undani wa ‘sakata’ hili kutoka kwa waandaaji wa tamasha hilo na vyombo vya ulinzi na usalama mkoa wa Mtwara ili kujuwa kinagaubaga kile kilichojitokeza