Latest Posts

WATAALAMU KUKUTANA MWANZA KUTAFUTA MWAROBAINI AINA MPYA YA MAGUGU MAJI ZIWA VICTORIA

Na Anania Kajuni.

Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Makamu wa Rais, na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wataalamu wa Uvuvi, Mazingira, Uchukuzi na Maji, viongozi wa Serikali na wadau mbalimbali wamepanga kukutana kutafuta mwarobaini wa changamoto ya aina mpya ya magugu maji iliyojitokeza katika Ziwa Victoria.

Timu ya wataalamu hao tayari ipo Jijini Mwanza ambapo siku ya Jumatatu wametembelea eneo la Kigongo/Busisi lilipo Daraja la Magufuli kwa lengo la kujionea aina mpya hiyo ya magugu maji ambayo imechukua nafasi katika eneo hilo na maeneo jirani.

Akizungumza mara baada ya kujionea hali halisi Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema wamehitisha kikao cha dharura kitakachofanyika Jumanne kikiwa na lengo la kujadili na kuja na suluhu ya tatizo hilo ambalo mpaka sasa bado halijapatiwa ufumbuzi.

“Suala la usafi kwenye miji yetu sio ombi tukiendelea kuomba ndo tunaona hali kama hii, sawa tumekutana Mwanza leo hii tutaangalia tatizo ni kubwa kiasi gani kesho tutakaa kikao cha haraka tutafute njia za haraka za kufanya hatuwezi kusema tufanye tafiti nyingi wakati hali ni mbaya,” amesema.

Hata hivyo Mhandisi Luhemeja amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala kuanzisha kampeni maalumu za kuhamasisha wananchi kufanya usafi katika miji au kaya zao.

“Kwahiyo mimi nitoe ombi kwa wakurugenzi wa Halmashauri na Makatibu Tawala tuanzishe kampeni maalumu ya kufanya usafi katika miji yetu na sasa hivi uchafu ni fursa unatengeneza Bioges, unafanyiwa urejeshaji lakini pia uchafu unatumika kutengenezea Kaboni,” amesema.

“Lakini pia Meneja NEMC Kanda ya Ziwa umesema vizuri kwamba kule Uganda wenzetu wamefanikiwa tutatuma baadhi ya watu wakimbie kule mara moja wakaangalie wao wamefanya nini tukopi na kuleta haraka kwa sababu inaathiri biashara kwa wananchi,” amesema Mhandisi Luhemeja

Awali Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza na timu hiyo ya viongozi, wataalamu na wadau wa mazingira amesema endapo magugu maji hayo hayatapatiwa mwarobaini yatapelekea athari kubwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuathiri mradi wa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

“Nafikiri ni jambo zuri Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi umekuja kwa sababu yeye anafahamu kwamba yale magugu yakianza kusambaa yakaenda kwenye mradi wa vizimba manayake jitihada za Rais Samia na uwekezaji wote ambao umefanyika hapo ziwani yote inakuwa ni kazi bure,” amesema.

“Kwa siku moja wamejaribu kuyatoa Magugu ukiyatoa leo tani 10 kesho yanazaliana tani 30 kwahiyo hakuna mjasiliamali mwenye uwezo wa kuyadhibiti magugu maji kwahiyo Samaki watakufa na uwekezaji mwingine ndani ya ziwa utakuwa ni mbaya,” amesema Mtanda

Mtanda amesisitiza timu hiyo kuhakikisha inaupatia mwarobaini changamoto kabla madhara makubwa hayajaanza kushuhudiwa.

“Ujio wenu ni faraja kubwa kwetu lakini ninacho sisitiza jambo hili linahitaji kushughulikiwa kwa haraka tukienda polepole kwa sababu inagusa watu wengi hususani kwenye kivuko tutachafuka sana,” amesema Mtanda

Afisa Mazingira Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO), Kitogo Laurence amesema aina mpya hiyo ya magugu maji inaathiri pia uzalianaji wa samaki hali ambayo inatishia pia afya za viumbe maji.

“Mimi nadhani ni wakati sasa wa wadau wote wa kukaa na kushirikiana na Serikali kama ambavyo Wizara zote tatu makatibu wakuu wake wapo kwahiyo tutaona namna ambavyo tunaweza kushirikiana kukabiliana na changamoto hii,” amesema.

Ameongeza kuwa “Kisayansi uwepo wa gugu maji unaathiri uzalianaji wa samaki, samaki wanazaliana kwenye maeneo ambayo yanaathiriwa na magugu maji lakini pia gugu maji linavyotanda inamaana wavuvi hawawezi kutandika nyavu zao wala kufanya shughuli zao za uvuvi tofauti na ilivyokuwa mwanzoni,”.

Mkazi wa Kigongo Feli lilipo Daraja la Magufuli, Yusuph Ndaki amesema uwepo wa magugu maji hayo umepelekea wavuvi kuhama eneo hilo kutokana na kuathiri shughuli za uvuvi.

“Lakini pia imepelekea hata kambi ya wavuvi kuhama kutoka eneo hili ambalo limezingilwa na magugu maji kwahiyo hiyo imekuwa ni changamoto sana kwao,” amesema Yusuph

Naye mmoja wa abiria ambaye pia ni mkazi wa Mkuyuni Jijini Mwanza, Monica Kamwina ameiomba Serikali kutatua changamoto hilo haraka iwezekanavyo ili kuwaondolea tatizo la kukaa muda mrefu kwenye kivuko.

“Haya magugu yameleta usumbufu sana kwa sisi abiria kwa sababu unajikuta unatumia gharama kubwa kwenye kuvuka lakini bado unakuja kukaa hapa kusubilia gari nalo livuke kwa awamu nyingine wakati wewe umewai kuvuka,” amesema Monica

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!