Clouds Media imekamilisha kilele cha tuzo za Malkia wa Nguvu kanda ya Kusini inayojumuisha mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa kuwapa tuzo malkia watano kwenye sekta mbalimbali usiku wa Oktoba 25 2024 kwenye ukumbi wa Police Officers Mess.Â
Washindi wa Malkia wa Nguvu Kusini- Mtwara ni pamoja na Mwanamke mwenye ushawishi tuzo aliyopewa Mwanaidi Sexbeti Mdendemi ambaye alipitia ubaguzi na manyanyaso baada ya mume wake kufariki (mwenye asili ya kiasia), hakupata mali, aliachiwa watoto watatu, maisha yaliharibika, akawa mlevi, lakini alifanikiwa kuanza maisha upya kwa kuuza maandazi kwenye beseni na sasa amekuwa mjasiriamali mwenye ushawishi sana Mtwara.
Â
Tuzo ya Biashara ya Chakula imeenda kwa Paulina Maivaji maarufu kama MC Pau ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi. Alianza biashara ya chakula kama mpika chips Wilayani Tandahimba, kwa sasa biashara yake imekua kubwa akiwa na uwezo wa kulisha sherehe tano mfulululizo na kwa pamoja.
Â
Upande wa Biashara ya Mapambo mshindi ni Martha Francis Chiwango, Mkurugenzi wa Martha Decorations yeye ni mfanyabiashara aliyejikita katika upambaji. Alianza safari yake ya mapambo kwa kujitolea kupamba kanisani na kwenye maharusi, baadaye akaanza kulipwa kwa kazi hizo, sasa ndiye mpambaji namba moja Lindi na Mtwara.
Â
Kwa upande wa Tuzo ya Mjasiriamali Bora mshindi ni Subira Kabula, maarufu kama Mama Sasuria, mmiliki wa shule za Sasuria Day Care and Primary Schools. Sababu ya kuanzisha day care ni baada ya kupata changamoto katika kumlea mtoto akaamua aanzishe sehemu ya kulelea watoto ambayo kwa sasa inaitwa Sasurea Day care and Primary Schools.
Â
Fidea Bright Ausi amekua Malkia wa Nguvu kwenye kipengele cha Ustawi wa Jamii. Yeye ni binti kutoka Mtwara ambaye akiwa mdogo, ameanzisha taasisi yake ya FB Empowerment nia na lengo ni kuwasaidia mabinti wa mikoa ya Kusini kupata nafasi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi ili waweze kuzikomboa familia zao. Ameweza kuwafikia wanawake zaidi ya laki moja huku akisaidiwa na taasisi mbalimbali nchini na za kimataifa.
Â
Mgeni rasmi kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma (Mwana FA) amewataka Malkia wa Nguvu kuwa sehemu ya mabadiliko chanya kwenye sehemu wanazoongoza akitoa mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan namna alivyobadilisha mwelekeo wa nchi kibusara, ujasiri na maono makubwa.
Â
Mbali na mgeni rasmi tuzo za Malkia wa Nguvu Kusini – Mtwara zimehudhuriwa pia na Kaimu Katibu Tawala Mkoa Mtwara, Manjiva Nzunda; Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya; Mstahiki Meya wa Mtwara. Shadida Ndile pamoja na wageni waalikwa mbalimbali.