Latest Posts

WATANZANIA KUNUFAIKA ZAIDI KUPITIA MFUMO WA USHIRIKIANO WA KAMPUNI, KUSHINDANA NA KAMPUNI KUBWA DUNIANI

Kampuni za Tanzania zaidi ya 100 zinatarajia kunufaika na mfumo wa ushirikiano wa kampuni ukijulikana kimombo kama franchise utakaziwesha kukuza biashara zao baada ya kupatiwa mafunzo ya pamoja yanayowakutanisha wadau mbalimbali wa ujasiriamali kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.

Hayo yamebainika siku ya Jumatatu Julai 22, 2024 kupitia kwa Gasper Mdee ambaye ni Mkuu wa Idara ya Programu kutoka Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF wakati wa siku ya kwanza ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema mafunzo hayo yanajulikana kama Empretec ambayo ni sehemu ya mradi unaotekelezwa na TPSF ikishirikiana na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) ukilenga kuwezesha biashara na kampuni za Kitanzania kukuza na kupanua biashara zao kwa kutumia mfumo wa Franchise.

“Kwa kupitia mradi huu, tunatarajia kwamba tunaweza kutengeneza ajira za moja kwa moja kwa watu elfu 30 na zile zisizo za moja kwa moja kwa watu zaidi ya elfu 50, mradi huu ulizinduliwa na ulianza kufanya kazi na kutekelezwa tangu mwaka 2021 na utatarajiwa kukamilika mwaka 2025” Ameeleza Mdee.

Aidha amesema kwamba wanatarajia kuwa na washiriki 40 kwa kundi la kwanza, na kufuata makundi mengine mawili ya watu arobaini arobaini, huku wakitazamia baada ya mafunzo hayo kukuza kampuni hizo na kuhakikisha mfumo wa francise unafuata kwa kuuza biashara zao ndani na hata nje ya nchi.

Amesema kuwa wafanyabiashara watakaojengewa uwezo wa kukuza chapa zao na kuuza duniani kote watasaidia katika ukuaji wa uchumi na kufanya nchi kuwa shindani kiuchumi.

“Baadhi ya kampuni ambazo zilianza ukuaji kwa njia hii ya ukasimishaji wa chapa za biashara (franchising) kwingineko ni kama Pepsi, Coca Cola, KFC ambapo Chapa zake zilikuwa zinauzwa na kueneaa duniani kote hali ambayo wafanyabiashara wa Kitanzania wanaanza kujengewa uwezo kufika huko” Ameeleza Gasper.

Kwa upande wake James Bulenzibuto, Mtaalamu wa Maendeleo ya Biashara wa Empretec katika programu ya AFRAP (African Franchise Accelerator Program) amesema malengo yao ni kuendeleza Franchise ndani ya Tanzania kwa kuchukua kampuni za Tanzania, kuzifundisha ujuzi wa kijasiriamali ili ziwe na uwezo mzuri katika kile wanachokifanya kwa kushirikiana na chapa ambazo tayari zinatambulika.

“Hizi siku sita za mafunzo tulizonazo, tunajihusisha na wajasiriamali, tunajaribu kuwasaidia wapate ujuzi zaidi wa kijasiriamali na tunataka kuhakikisha kwamba tunawasaidia kuendeleza biashara zao ili zivutie zaidi kwa wateja” Ameeleza Bulenzibuto.

Amesema kwamba wahudhuriaji wa mafunzo hayo watafaidika sana kwani njia zitakazotumika zitabadilisha mtazamo wao wa namna ya kufikiri na kutenda itakayowawezesha kufanikiwa zaidi

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamekuwa na matumaini makubwa ya kufaidika nayo kwa kukuza zaidi biashara na kujifunza mbinu mpya kutoka kwa kampuni zingine. Geofrey Kidindima ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Makika Trinity Enterprises amesema kwamba mafunzo hayo yataenda kuwabadilisha mtazamo wa kutofanya kazi Tanzania pekee bali na sehemu zingine za dunia.

Naye mwanzilishi wa taasisi ya Thamani Afrika Solutions, Mary Marealle amesema kwamba mafunzo hayo yatamuwezesha kuongeza ujuzi wa huduma yake ya kuongeza thamani kupitia duka la pamoja kupitia program ya kushirikiana (Franchise) ambapo Watanzania wengi watanufaika.

Mfumo wa franchise ni mfumo wa biashara ambapo mmiliki wa biashara au kampuni hutoa leseni au ruhusa kwa mtu au kampuni nyingine kutumia jina lake, bidhaa, huduma, na mfumo wake wa biashara. Hii inaruhusu kampuni kuanzisha biashara yao kwa kutumia mfano wa biashara uliofanikiwa na kujaribiwa.

Kwa kutumia Tanzania kama majaribio tangu mwaka 2021, mfumo huu unatarajiwa kuleta ushirikiano wa kiuchumi wa haraka zaidi, diplomasia ya kibiashara, uhamisho wa haraka wa ujuzi, uundaji wa ajira, uzalishaji mali, na kupunguza umasikini barani Afrika.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!