Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amehimiza Watanzania kuchukua hatua za haraka kushirikiana na wafanyabiashara kutoka taifa la China ili kukuza wigo wa kibiashara na kupata fursa zaidi.
Prof. Kitila ameyasema hayo siku ya Jumanne Julai 30, 2024 baada ya kuzungumza kwenye Kongamano la Biashara na Uwekezaji Baina ya Tanzania na China ambapo ameeleza kuwa serikali inaendelea kuwaalika wawekezaji kutoka taifa la China na mataifa mengine kutokana na uwepo wa mazingira mazuri na fursa mbalimbali zilizopo nchini hivyo Watanzania ni muhimu kuchangamkia fursa ya ushirikiano huo.
“Nitoe wito kwa Watanzania wafanyabisahara na wawekezaji wachangamkie fursa za wageni kama hawa ili washirikiane watengeneze partnership (muungano wa kibiashara) watapata mtaji na watapata teknolojia” Ameeleza Prof. Kitila.
Aidha ameeleza kuwa serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuwaunganisha Watanzania pamoja na kampuni za kiwekezaji ili Watanzania wakuze kipato chao na taifa kwa ujumla.
“Tumeweka utaratibu mzuri wewe Mtanzania kama una ardhi tunakuunganisha na kampuni binafsi kutoka nje ili mshirikiane, wewe una mtaji wa ardhi yeye ana fedha na teknolojia, mnashirikiana kwa ajili ya kuweza kufanya uwekezaji” Amesema Prof Kitila.
Katika hatua nyingine amesisitiza watu kuachana na imani potofu kuwa bidhaa zinazozalishwa na taifa hilo hazina ubora mzuri kwani bidhaa zote zinazoingia nchini na kuzalishwa zinakaguliwa kuangaliwa kuwa na ubora unaokidhi.
Aidha, Prof. Kitila ameeleza kuwa dira ya taifa kwa kiasi kikubwa inaangazia eneo la mageuzi ya uchumi (Economic Transformation) hivyo ni muhimu kwa nchi kuvutia na kukuza uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi kwa maendeleo ya nchi.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini China, Balozi Hamis Omar amesema ameleta ujumbe wa Wawekezaji takribani 100 kutoka nchini China kutafuta fursa za uwekezaji kwa kushirikiana na Watanzania na kwamba wamekuja kutafuta fursa kwenye maeneo mbalimbali ya sekta ya viwanda na madini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Gilead Teri ameeleza kuwa TIC kwa kushirikiana na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) watashirikiana kuwawezesha wawekezaji hao kuwekeza kwenye viwanda, usindikaji wa mazao (Kahawa na Katani), nishati jua, madini, tehama na ujenzi.