Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewataka Watanzania kutumia takwimu zinazozalishwa na ofisi hiyo kwani ndizo zinazotumika katika mipango ya serikali na kupanga mikakati ya Taifa.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa takwimu za uchumi Daniel Masolwa Katika maonesho ya Nanenane yaliyopo Nzuguni Jijini Dodoma.
Masolwa amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya takwimu sura na 351 ndiyo yenye dhamana ya kutayarisha takwimu rasmi nchini ambazo zinatakiwa zitumike katika kupanga mipango ya maendeleo, kufanya ufuatiliaji lakini pia kutathmini utekelezaji wa programu mbalimbali za kitaifa na za kimataifa.
“Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndio chanzo pekee cha uhakika wa takwimu ambazo zinatakiwa zitumike kutupeleka mbele, hizi takwimu zingine za vichochoroni ambazi hazijakidhi viwango na ambazo hazijafuata miongozo ya kimataifa tuachane nazo, Ofisi ya Taifa ya Takwimu ipo kwa ajili ya kutupatia takwimu za uhakika na kwa ajili ya maendeleo endelevu”, ameeleza Masolwa.
Katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa aliwataka kuhakikisha wanajiandikisha katika maeneo yao na kupata kadi ya mpiga kura ili kutimiza wajibu wake kama mwananchi na haki yake ya kikatiba.
“Natoa wito kwa wananchi wote popote walipo wahakikishe kwamba fursa hii hawaipotezi kwa kupiga kura mwaka huu lakini pia katika uchaguzi mkuu mwakani”, amesema.
Ameongeza kuwa katika uchaguzi unachagua kiongozi ambaye atakusaidia kukuongoza wewe lakini pia kufanikisha malengo ya mwananchi.
“Tunajua wazi kwamba umri wa mpiga kura mwenye sifa ni kuanzia miaka 18 na kuendelea na kutokana na takwimu za Sensa za Mwaka 2022 zinaonesha idadi ya hao wapiga kura kwa kila kata, kila wilaya na kila mkoa kwa hivyo tujitokeze”, ameeleza.