Latest Posts

WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU WAHOJI MAUAJI YA ALBINO KUWA MENGI KIPINDI CHA UCHAGUZI

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) pamoja na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wameeleza kusikitishwa na tukio la utekwaji na mauaji ya kikatili kwa mtoto mwenye ualbino Asimwe Novath (2) mkazi wa kata ya Kamachumu wilaya ya Muleba mkoani Kagera huku wakilitaka Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio.

Kulingana na taarifa ya mashirika hayo yanayochechemua haki za binadamu Tanzania iliyotolewa Jumatano Juni 19, 2024, tukio hilo ni ukiukwaji wa wazi wa sheria na makubaliano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.

“Tukio hili ni ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977; Inabainisha ulinzi wa haki ya kuishi, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu 2006, Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, na Mikataba ya Kimataifa ya Haki za Binadamu pamoja na sheria za nchi ikiwamo Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura Namba 16 (Marejeo ya 2019). THRDC na LHRC inalaani vikali vitendo hivi vya kikatili, kinyama na kihuni dhidi ya ndugu zetu wenye ualbino” Imeeleza taarifa hiyo.

Wadau hao wameonesha wasiwasi wao wa kuongezeka kwa matukio mithili ya hayo hasa wakati ambao Taifa la Tanzania linaelekea kufanya  uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi mkuu.

“Ni wazi kuwa mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino yamerudi kwa kasi katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi hasa kwa watoto, itakumbukwa mwaka 2015 mkoani Rukwa kulitokea tukio la kushambuliwa kwa mtoto wa kiume aitwaye Baraka Cosmas mwenye umri wa miaka sita (6) akiwa amelala na mama yake mzazi ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumbani kwao na kumkata kiganja” Imeeleza taarifa.

Mbali na kulitaka Jeshi la Polisi kuchunguza matukio hayo, THRDC NA LHRC wameitaka Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) kuweka mikakati madhubuti ya kuwatambua na kusimamia ustawi wa watu wote wenye ualbino katika maeneo yote nchini na Bunge la Tanzania kutumia kipindi hiki cha Bunge la bajeti kujadili na kuweka fungu maalumu ili kuimarisha mifumo ya ulinzi kwa watu wenye ualbino kuanzia ngazi ya Kitongoji, Kijiji, Kata, Wilaya, Mkoa na Kitaifa ili kuhakikisha maisha ya watu wenye ualbino yanalindwa na watu hao waendelee kufurahia maisha kama watu wengine katika jamii.

Aidha Jamii imetakiwa kuachana na imani potofu juu ya matumizi ya viungo vya watu wenye ualbino kwa kuhusisha na utajiri au kujipatia mamlaka katika ngazi mbalimbali.

“Tunawahimiza wanajamii wote kusimama pamoja kuibua na kutoa taarifa juu ya watu wote wanaofanya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa sababu ya imani za kishirikina” Wameeleza wadau hao.

Itakumbukwa kwamba, mnamo tarehe 30 mwezi Mei, 2024 kuliripotiwa tukio la kutekwa kwa Asimwe Novati lililofanywa na watu wasiojulikana katika Kijiji cha Bulamula, Kitongoji cha Mbale, Kata na Tarafa ya Kamachumu wilayani Muleba mkoani Kagera. Siku ya tarehe 30 mwezi Mei, 2024 iliripotiwa kuwa watu hao walimvamia kwa kumkaba mama wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Kebyera Richard, kisha kumchukua na kukimbia na mtoto huyo kusikojulikana. Siku ya tarehe 17 Juni, 2024 iliripotiwa kupatikana kwa mwili wa mtoto huyo ukiwa umekatwa viungo vyake ikiwamo mikono, ulimi na macho.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Muleba Benjamini Mwakasyege, mwili huo ulikutwa umetelekezwa kwenye karavati yenye maji ya barabara ya Makongora, kijiji cha Malele.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!