Mkuu wa wilaya ya Nzega Bi. Naitapwaki Tukai ameanza kutoa mahitaji ya shule kwa wanafunzi wanaotoka kwenye mazingira duni wilayani hapo ili kuwaondolea mkwamo watoto hao wa kutohudhuria masomo kutokana na wazazi wao kushindwa kununua mahitaji hayo.
Akigawa sare za shule, madaftari, kalamu, rula na mikebe kwa baadhi ya wanafunzi walioambatana na wazazi wao ofisini kwake, amewataka pia wazazi wengine walioshindwa kununua mahitaji hayo kuwaleta watoto wao kwa ajili ya kuchukua vifaa hivyo.
“Rais amejenga miundombinu ya shule hivyo tunapaswa kumuunga mkono kwa kuwasaidia mahitaji ya shule watoto wasiojiweza ili wasikwame”, amesema Bi. Naitapwaki.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi ambao wamefika kupatiwa mahitaji hayo akiwemo Magreth James na Johari Petro, wamemshukuru mkuu huyo wa wilaya na kubainisha kuwa watoto watawapeleka shule kutokana na kupata mahitaji hayo.
“Tunakushukuru sana mkuu wetu wa wilaya kwa kuligundua hilo katika familia zetu na kuamua kutusaidia mahitaji haya, hivyo watoto wetu tunaenda kusoma maana tulikua tunajiuliza tunawakamilishiaje mahitaji ya shule ingalipo shule tayari zimeshafunguliwa”.
Mikakati hiyo ni miongoni mwa jitihada za kukabiliana na mdondoko wa elimu mkoani humo unaosababishwa na baadhi ya familia kutomudu gharama za mahitaji ya shule.