Latest Posts

WATUMISHI WA SERIKALI MKOANI MTWARA WAPATIWA MAFUNZO KUHUSU SHERIA YA UNUNUZI WA UMMA

Wizara ya Fedha imeandaa mafunzo ya siku moja kwa watumishi wa serikali kutoka sekta mbalimbali mkoani Mtwara, ili kuwaelimisha kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Mafunzo hayo yamefanyika Septemba 6, 2024, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani, ambapo mada kuu zilizowasilishwa ni pamoja na fursa zinazopatikana ndani ya sheria hiyo.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Ununuzi wa Umma (PPRA) Kanda ya Kusini, Fenias Manasseh, alieleza kuwa lengo la mafunzo haya ni kuwasaidia watumishi wa serikali wanaohusika na michakato ya ununuzi kuelewa mabadiliko ya sheria, ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za maendeleo zinazotolewa.

“Hapa waliopo ni taasisi nunuzi zinazohusika moja kwa moja na michakato ya ununuzi. Ni muhimu wakifahamu mabadiliko yaliyopo kwenye sheria ya ununuzi wa umma ili waweze kutumia fursa nyingi zinazopatikana kupitia sheria hii,” alisema Manasseh.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Flora Tenga, alieleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu kwa maofisa mipango na viongozi kuhusu fursa zilizopo kwenye sheria hiyo na namna ya kuzitekeleza. Aliongeza kuwa sheria ya ubia kati ya sekta hizi imefungua milango kwa wawekezaji kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mikataba ya ubia.

“Mafunzo haya yatawasaidia viongozi kuelewa fursa zilizopo kwenye miradi ya ubia, ambapo badala ya kutegemea fedha za serikali peke yake, wanaweza kutumia sheria hii kumwalika mbia mwekezaji kuchangia miradi ya maendeleo, hususan kwenye Halmashauri zetu,” alisema Tenga.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mtwara, Abdillah Mfinanga, alisisitiza kuwa mafunzo haya yanasaidia katika kutatua changamoto mbalimbali zinazohusu utekelezaji wa sheria ya ununuzi wa umma, na hivyo kusaidia katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi zaidi.

Mafunzo hayo yamelenga kutoa mwongozo sahihi kwa watendaji wa serikali katika ngazi za mikoa, wilaya, na Halmashauri kuhusu matumizi bora ya sheria mpya ya ununuzi wa umma ili kuleta maendeleo kwa taifa.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!