Latest Posts

WAUMINI WASHANGAA UKIMYA WA ASKOFU MALASUSA SAKATA LA MAUAJI NA UTEKAJI NCHINI

Mwanaharakati wa haki za kijamii nchini Tanzania Godlisten Malisa, amelitaka Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuzungumza hadharani dhidi ya vitendo vya utekaji na mauaji vinavyoendelea nchini.

Katika ujumbe wake wa wazi aliouchapisha kupitia jukwaa la mtandao wa X kwa Baba Askofu Dkt. Alex Malasusa ambaye ni mkuu wa KKKT, Malisa ameomba kanisa hilo kutumia sauti yake yenye nguvu kulaani matendo hayo.

“Je, lini litatumia sauti hiyo kukemea maovu yanayoendelea? Kanisa linawezaje kuona mtu akishushwa kwenye basi na kuuawa kikatili na likakaa kimya?” amehoji Malisa, akieleza umuhimu wa KKKT kuchukua msimamo thabiti dhidi ya matukio haya ya kikatili.

Katika andiko lake, Malisa amepongeza Kanisa Katoliki kwa msimamo wake thabiti wa kukemea uovu bila woga.

“Kuna makanisa yakiwaona viongozi wa serikali point zote za kukosoa zina-evaporate, wanaishia kujichekesha na kusifia. Lakini si kanisa katoliki, kamwe. Katoliki hata umuite Askofu Ikulu, atakuja, atakunywa juice yako na “atakuchana” bila kupepesa macho”, alisema, akisisitiza ujasiri wa Kanisa Katoliki katika kukemea maovu mbele ya viongozi wa serikali.

Malisa pia amekumbusha kuwa imani ya Kikristo inapaswa kutetea haki za kila mtu, bila kujali dini au kabila. “Neema si kwa Walutheri pekee bali kwa watu wote. Ndio maana katika Kateksimo yake aliandika ‘Et alias oves habeo’ akimaanisha na kondoo wengine ninao ambao si wa zizi hili. Nao wanastahili neema,” amesisitiza Malisa, akinukuu maandiko ya Martin Luther na kuonesha kuwa sauti ya kanisa inapaswa kusimama kwa ajili ya haki ya kila mmoja.

Akimkumbuka Baba Askofu Shoo kwa msimamo wake wa kukemea uovu bila hofu, Malisa alitoa wito kwa KKKT kuendelea na roho ile ile ya kupinga maovu. “Tunaomba usimzimishe roho aliyekua na Kanisa kipindi cha Askofu Shoo,” alisema, akionesha matumaini kuwa tamko rasmi la KKKT linaweza kuokoa roho nyingi.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!