Mbunge wa Jimbo la Nanyamba Abdallah Chikota amewaomba wazazi na walezi kuwapeleka watoto wao shule ili waweze kupata elimu itakayowasaidia katika maisha yao ya baadae.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa shule ya msingi Nyundo B iliyopo Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara katika Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025 Chikota amewahimiza wazazi kuwapeleka watoto shule ili waweze kupata elimu na kuongeza maarifa.
“Shule hii majengo haya yasiwe kama mapambo tunataka watotot wajae madarasani kwahiyo tuwapeleke watoto wetu serikali imeshatimiza wajibu wake watoto wenu wanabahati wameanza kusoma mpaka shule ya msingi kuna umeme.”Amesema Chikota
Kwa upande wake Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ally Usi amewataka kutunza miundombinu ya shule hiyo ili iweze kuwanufaisha na kuwaletea mafanikio wakazi wa eneo hilo.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Nanyamba Saidi Nanyembe amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza uandikishaji wa wanafunzi wa awali na darasa la kwanza ukilinganisha na miaka iliyopita pamoja na kupunguza utoro kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa mradi huo wa shule ya msingi Nyundo B umegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 300 na pesa zilizobaki ni zaidi ya milioni 7 ambazo zitapangiwa shughuli nyingine.
Sambamba na hilo Mkimbiza Mwenge wa Uhuru Ismail Ally Usi amewataka wananchi kuendelea kulinda amani,umoja,mshikamano na utulivu uliokuwepo pamoja na kujitokeza kupiga kura wakati utakapofika.