Mkurugenzi wa Huduma ya Daughters and Sons of Jerusalem, Mwl. Joyce Kisha, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha katuni wanazowaonesha watoto kupitia runinga, simu janja au tablet zinazingatia maadili mema na kuwajengea watoto uwezo wa kujitambua.
Akizungumza katika semina maalum kwa watoto na wazazi jijini Dodoma, Mwl. Kisha alisema watoto wengi wa kizazi cha sasa wanapokea maarifa kupitia mitandao na vipindi vya katuni visivyokuwa na maudhui sahihi ya kimalezi, hali inayochangia mmomonyoko wa maadili na kushindwa kutofautisha jema na baya.
“Nataka mtoto akiwa na tablet au simu ajue hiki ninachoangalia kitamsaidia kujitambua. Huu siyo ujeuri, bali ni kujenga uwezo wa kufahamu lipi ni jema na lipi si sahihi. Hii ndiyo silaha ya kuwakuza watoto katika dunia ya sasa,” alisema.
Watoto Wajifunze Kujitambua kwa Kuongozwa na Maadili
Mwl. Kisha alitoa mfano wa baadhi ya katuni zinazorushwa kwa watoto ambazo huonesha vitendo visivyofaa kwa umri wao, kama mabusu au mahusiano ya kimapenzi, akisisitiza kuwa watoto wanapaswa kufundishwa kutambua kuwa maudhui hayo hayawafai kwa hatua ya ukuaji walipo.
“Kuna katuni unakuta watu wanabusiana au kufanya mambo ya mahusiano — si sawa. Mtoto anapaswa kuambiwa, hii si ‘level’ yako, hujafikia umri huo,” alieleza kwa msisitizo.
Wito kwa Wazazi Kuwajibika kwenye Malezi
Katika hotuba yake, Mwl. Kisha pia aliwataka wazazi wasiwaachie wadada wa kazi jukumu la msingi la malezi ya watoto wao, akisisitiza kuwa mzazi anapaswa kushiriki moja kwa moja katika kila hatua ya malezi, ikiwemo kuchunguza mavazi wanayovaa watoto wao.
“Hivi kweli mama hujui wiki nzima mwanao alivaa nini? Ni muhimu kuchukua muda kumvalisha mtoto wako ili ujue anachovaa na kwa hali hiyo unakuwa karibu naye kiakili na kihisia,” alisema.
Huduma ya Daughters and Sons of Jerusalem Yajikita kwenye Maadili
Huduma ya Daughters and Sons of Jerusalem, inayoongozwa na Mwl. Kisha, inalenga kuwajengea watoto na vijana uwezo wa kubadilika kifikra na kitabia, hasa katika zama hizi za matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa Mwl. Kisha, shirika hilo linatoa semina na mafunzo ya maadili, elimu ya uzazi kwa vijana, matumizi salama ya teknolojia, pamoja na uongozi kwa watoto na vijana ili kuwajengea msingi imara wa maisha ya baadaye.