Latest Posts

WAZEE WAASISI CCM WASHIKWA MKONO LUDEWA, WAPEWA SUKARI NA SABUNI

News, Njombe.

Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Njombe imefanikiwa kuwashika mkono kwa kuwawezesha vitu mbalimbali ikiwemo sukari na sabuni wazee ambao ni waasisi wa chama hicho wanaoishi kata ya Mavanga wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Akikabidhi zawadi hizo Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Gelard Mpogolo amesema wameamua kutoa zawadi hiyo ndogo ili kuwaenzi na kuwaonesha thamani kutokana na kazi kubwa ya kujenga chama waliyoifanya.

Vile vile Viongozi wa CCM chini ya Jumuiya ya Wazazi mkoa wa Njombe wamefika shule ya sekondari Mavanga na kushiriki zoezi la kupanda miti kuzunguka eneo la shule ya Sekondari na kutoa mada mbalimbali kwa wanafunzi ikiwemo ukatili huku Jolam Hongoli mjumbe wa kamati ya utekelezaji Jumuiya ya wazazi akiwasisitiza kuzingatia nidhamu kwani ndiyo itawasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.

Kwa upande wake Afande Neema Lutufyo, Kaimu Mkuu wa Dawati la Jinsia wilaya ya Ludewa na Rabson Mahenge, Mjumbe Baraza la wazazi CCM Taifa mkoa wa Njombe wamesema vitendo vya ukatili, ushoga na usagaji vinatokana na kukengeuka kimaadili tangu wadogo jambo ambalo elimu inatakiwa kutolewa kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM mkoa wa Njombe Gelard Mpogolo pamoja na katibu wake Emmanuel Ngulugulu wamesema kazi kubwa ya jumuiya ya wazazi ni kuelekeza maadili mema kwa jamii na ndiyo sababu ya kufika katika shule hiyo na kuzungumza nao.

Samuel Haule na Faraja Mgina ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mavanga ambao wameahidi kuendelea kuzingatia masomo kama walivyofanya watangulizi wao kidato cha nne kwa kuwa shule ya kwanza kwa wilaya ya Ludewa huku Joseph Mapunda, Mkuu wa Shule hiyo akishukuru kwa elimu iliyotolewa na zawadi mbalimbali.

Latest Posts

Don't Miss

Stay in touch

To be updated with all the latest news, offers and special announcements.

error: Content is protected !!