Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa wito kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, akibainisha fursa kubwa iliyopo katika utoaji wa huduma na manunuzi ya bidhaa migodini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa Chama cha Watoa Huduma na Wasambazaji wa Bidhaa Migodini (TAMISA) jijini Dar es Salaam, Waziri Mavunde alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya shilingi trilioni 3.1 zimetumika kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma migodini.
“Uwekezaji nchini Tanzania katika sekta ya madini unakua kila siku kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na serikali chini ya uongozi wa Mh. Rais Dkt. Samia S. Hassan,” alisema Mavunde.
Aliongeza kuwa chama hicho kitaimarisha uwezo wa watanzania ili kuwa washindani katika utoaji wa huduma migodini, na alieleza kuwa anatamani kuona fedha hizo zinabaki mikononi mwa Watanzania kwa lengo la kuchochea uchumi kupitia kuanzisha viwanda vya kuzalisha bidhaa zinazohitajika migodini.
Waziri Mavunde aliwapongeza TAMISA kwa kuanzisha chama hicho kama alivyoagiza na alitarajia kuwa kitakuwa jukwaa la mafanikio kwa sekta binafsi Tanzania. “Natamani sana kuziona hizi trilioni 3.1 zinabaki mikononi mwa Watanzania ili kuchochea uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza Waziri Mavunde.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TAMISA, Peter Kumalilwa, alisema kuwa chama hicho kinalenga kuwaleta pamoja watoa huduma na wasambazaji wa bidhaa migodini, pamoja na kuishauri serikali kuhusu namna bora ya kujenga uwezo wa Watanzania kunufaika na sekta ya madini. Alieleza kuwa chama hicho pia kitashirikiana na serikali katika kutatua changamoto zinazohusiana na suala la Local Content.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TPSF, na Mwenyekiti wa Kongani ya Huduma, Octavian Mshiu, alipongeza juhudi za serikali za kuvutia uwekezaji na kukuza sekta binafsi nchini, akiahidi kuwa TPSF itashirikiana na wadau wote kuhakikisha Watanzania wanachangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na sekta ya madini.