Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Ijumaa Julai 05, 2024 amezindua Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) na kuahidi kuwa Serikali itafanya nayo kazi kwa karibu ili iweze kufanikisha malengo ya Tanzania kufanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo kwenye hafla iliyofanyika katika hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, Majaliwa amesema Serikali ina imani kubwa na kamati hiyo kwamba itapata mafanikio.
“Tuambieni tufanye nini ili tuwe mabingwa, kusanyiko hili liibue nini tufanye sasa na tuanze leo kufanya maandalizi. Tumeunda kamati yenye weledi na wataalamu kwenye sekta ya michezo, tunategemea itupeleke kwenye mafanikio makubwa. Uwepo wenu ni imani ya Serikali kwamba mnaweza kusimamia suala hili.” Amesema Majaliwa.
Amesema kuwa Serikali imeendelea kufanya maandalizi ikiwamo maboresho ya miundombinu ya viwanja, barabara, reli, anga na usafiri wa maji.
“Serikali tumejiweka vizuri kuwa mwenyeji wa mashindano haya; sifa, uwezo na dhamira ya kufanikisha mashindano haya tunayo,” Amesisitiza Majaliwa.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amesema kuwa mashindano hayo yataongeza idadi ya wageni na watalii hapa nchini ambao watakuja kwa ajili ya kutazama mashindano na matukio yanayohusiana na AFCON 2027 hivyo kusaidia kuongeza mapato ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema kuwa uzalendo na utashi wa kisiasa wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umeifanya sekta ya michezo kusonga mbele na hatimaye kuiheshimisha sekta ya michezo nchini.
Amesema kuwa Kamati hiyo itakuwa na kamati ndogo 13 za wataalamu na watu waliobobea katika maeneo mbalimbali ambayo ni miundombinu, mawasiliano, fedha, tiba na kinga, usafiri, ulinzi na usalama, sheria, masoko, matangazo, uendeshaji matukio, usimamizi wa timu, mashabiki na watazamaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema kuwa Serikali imeweka mpango wa kushiriki michuano ya AFCON kwa miaka mitatu mfululizo na ametoa wito kwa kamati inayoongozwa na Leodgar Tenga isaidie Tanzania kufuzu michuano ya AFCON 2025 ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya AFCON 2027 Leodgar Tenga amesema kuwa kamati hiyo itafanya kile kinachostahili ili nchi iweze kufanikiwa na kufanya vizuri katika michuano ya AFCON 2027 huku akiipongeza serikali kwa kwa kuhusisha watu makini kwa ajili ya kufanikisha AFCON 2027.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Walace Karia ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa michezo ikiwamo kuweka mazingira rafiki ya kuendesha shughuli za michezo nchini.